Jumatatu, Agosti 05, 2013

MAREKANI NA UINGEREZA ZAGOMEA MATOKEO YA URAIS ZIMBABWE

Marekani na Uingereza ambazo ziliiwekea Zimbabwe vikwazo vya kiuchumi zimeelezea kusikitishwa na matokeo yaliyompa ushindi Rais Robert Mugabe kuliongoza tena taifa hilo kwa miaka mitano ijayo.

Mugabe alizoa kura 2,110,434 ambazo ni sawa na asilimia 61 ya jumla ya kura zote huku Kiongozi wa MDC-T, Morgan Tsvangirai akiambulia asilimia 34. Tayari Tsvangirai amepinga matokeo hayo.
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi Zimbabwe, ushindi wa Zanu-PF unafanya chama hicho kuwa na asilimia kubwa ya wabunge.
Tsvangirai amezoa viti 50 wakati viwili vimetwaliwa na wagombea binafsi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry alisema Uchaguzi wa Zimbabwe ulikuwa na rafu nyingi na kumpa ushindi Mugabe.
“Uchaguzi haukufuata taratibu zinazotakiwa kama ilivyoelezwa na waangalizi wa ndani na Marekani haitaki kuamini kama matokeo yaliyotangazwa kama yanarandana na ushindi wa Mugabe na watu wa Zimbabwe,” alisema Kerry.

“Pamoja na Marekani kutokupewa nafasi ya uangalizi, lakini tunaweza kusema matokeo yaliyotangazwa yamejaa udanganyifu,” alisema.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, William Hague alielezea masikitiko yake hasa baada ya Robert Mugabe kutangazwa mshindi kwa muhula mwingine.
Katika taarifa yake iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza, Hague alisema: “Dunia nzima ilikuwa ikiiangalia Zimbabwe, wakati Tume ya Uchaguzi ikitangaza ushindi wa Mugabe.
“Nawataka wananchi wa Zimbabwe kubakia watulivu. Hata hivyo, hatuafikiani sana na matokeo haya.”
Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia, Bob Carr alisema, kilichofanyika kimeshapita.
“Hii inaonyesha ni wazi watu wengi hawakupiga kura na haileti upatanisho sawia na wa ushindi,” ilisema taarifa hiyo.

0 comments:

Chapisha Maoni