Serikali ya Rwanda imetoa tamko linaloonyesha kutoielewa kauli
ya Rais Jakaya Kikwete, iliyoamuru wahamiaji haramu kuondoka nchini,
hali inayoonekana kukwepesha hoja.
Rwanda kupitia waziri wake wa Mambo ya Nje,
Louise Mushikiwabo, ilikaririwa ikieleza kwamba hawatajibu mapigo agizo la Rais Jakaya Kikwete ya kuwataka Wanyarwanda wote waliolowea Magharibi mwa Tanzania kuondoka haraka.
Louise Mushikiwabo, ilikaririwa ikieleza kwamba hawatajibu mapigo agizo la Rais Jakaya Kikwete ya kuwataka Wanyarwanda wote waliolowea Magharibi mwa Tanzania kuondoka haraka.
Mushikiwabo alisema wako tayari kuwapokea na
kuwalinda wote waliofukuzwa Tanzania kwa kisingizio kuwa ni wahamiaji
haramu, akieleza kwamba anasikitishwa kwa kuwa Tanzania haikufanya
jitihada yoyote kuwasiliana na Rwanda kuhusu suala hilo kabla ya
kuchukua uamuzi huo.
“Ni uamuzi ambao umeshachukuliwa,
hatukushirikishwa kwa namna yoyote na jukumu letu kama serikali na taifa
ni kuwahakikishia ulinzi wote wanaokuja, na hili ndilo suala
tunalolishughulikia kwa sasa,” alisema.
Kwa mujibu wa gazeti la New Times, Mushikiwabo
aliwaeleza waandishi wa habari kwamba agizo hilo la Rais Kikwete pamoja
na ushauri wa kuitaka Serikali ya Rwanda kuzungumza na wanamgambo hasimu
wa FDLR waliopo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), hayatayumbisha
uhusiano imara baina ya Watanzania na Wanyarwanda.
“Sisi si majirani tu, tuna mfungamano imara baina
ya watu wetu pia, tuna mfungamano wa damu, wa kibiashara, na mengine
mengi ya kutufanya tuendelee kuwa pamoja,” alisema na kutumia fursa hiyo
kuwakaribisha Watanzania nchini Rwanda.
Watanzania wanaweza kuishi hapa kwa umri wowote
wanaotaka. Tunawachukulia kuwa ni watu wetu muhimu kwenye fungamano la
Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisisitiza.
Rais Kikwete wakati akihitimisha ziara yake mkoani
Kagera alitoa agizo la kuwataka wanaomiliki silaha kinyume cha sheria
na wahamiaji haramu ama kuondoka au kuhalalisha ukazi wao, huku akitoa
wiki mbili kwa zoezi hilo kutekelezwa, kabla ya kuanza kwa operesheni ya
kuwasaka watu hao.
Kauli hiyo ilitokana na kushamiri vitendo vya
kihalifu katika eneo la Kanda ya Ziwa, Rais hakutaja jina la nchi ya
wahamiaji hao. Kwa ukanda huo Tanzania inapakana na Kenya, Uganda,
Rwanda, Burundi na DRC.
Pia, Rais Kikwete katika hotuba yake ya mwisho wa
mwezi alizungumzia kusikitishwa na kauli za shutuma, kejeli na
udhalilishaji zilizotolewa na Rais Paul Kagame wa Rwanda dhidi yake.
Mvutano baina ya Rwanda na Tanzania ulianza
kuwekwa hadharani Mei mwaka huu, baada ya Rais Kikwete kuishauri Rwanda
kukaa na kuzungumza na FDLR wenye makao yao DRC, hatua ambayo
haikuifurahisha Serikali ya Rwanda.
Wakati Rwanda ikieleza hayo jana Katibu Mkuu
Kiongozi, Ombeni Sefue alizungumza na gazeti hili, na kutaka majibu ya
kauli hiyo ya Rwanda yatolewe na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa.
0 comments:
Chapisha Maoni