Alhamisi, Agosti 08, 2013

MUME WA ZAMANI AANZA MBWEMBWE KWA WASTARA JUMA BAADA

MIEZI nane baada ya kufariki dunia mumewe Juma Kilowoko ‘Sajuki’, hatimaye mume wa pili wa staa wa filamu za Kibongo, Wastara Juma aitwaye Ahmed Kushi ameibuka na kudai kwamba anatambua kwamba staa huyo bado ni mkewe na anataka ampatie mwanaye aliyezaa naye.

Kwa muda mrefu kulikuwa na taarifa kuwa Wastara aliachana na mwanaume huyo kwa talaka kabla ya kuolewa na Sajuki lakini kuibuka kwake na madai kuwa bado mwanadada huyo ni mkewe kumezua mshangao mkubwa.

MADAI YA KUSHI
Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni, Kushi alifunguka kwa mara ya kwanza kuwa yeye na Wastara walifunga ndoa ya Kiislamu mwaka 2000 na kujaliwa kupata mtoto mmoja wa kiume aitwaye Fares.
Alisema: “Kisheria bado ni mke wangu kwa kuwa nilikuwa nimempa talaka moja tu wala hazikufika tatu,” alisema Kushi na kudai kwamba ndoa yake na staa huyo ilidumu kwa mwaka mmoja na nusu na kuvunjika kutokana na kutawaliwa na migororo.
Jamaa huyo alidai kuwa zaidi ya mara tatu amekuwa akimtaka Wastara ampatie mwanaye huyo ambaye kwa sasa ametimiza miaka minane bila ya mafanikio.


KWA NINI WAKATI HUU?
Gazeti hili liliamua kumbana kwa kumuuliza kwa nini ameibuka wakati huu baada ya Sajuki kufa na mbona hakujitokeza kwa zaidi ya kipindi cha miaka kumi iliyopita? Pia akaulizwa kwa nini ameamua kutafuta umaarufu kwa kumdhalilisha? Akaishia kukaa kimya.

WASTARA AFUNGUKA
Baada ya Kushi kuibuka na ishu hiyo yenye utata, gazeti hili lilizungumza na Wastara ambapo alikuwa na haya ya kusema:
“Kuhusu mtoto, kama kweli alikuwa na lengo la kumchukua mwanaye na ananijua, basi atakuwa anawajua wazazi wangu hivyo angefuata utaratibu.
“Hakuna utaratibu kama huo kama kweli anamhitaji mwanaye angeenda kwa wazazi wangu, huko ni kunidhalilisha kwa kuwa ananiona mnyonge baada ya kufiwa na mume wangu Sajuki.
“Kama siyo kunidhalilisha ni nini? Naomba asitumie jina langu kutafuta umaarufu kwa kunichafua. Naomba aache kwa sababu ananiongezea maumivu juu ya maumivu.”
Kuhusu madai kwamba bado ni mkewe, Wastara alilia: “Hivi huyo mtu alikuwa wapi muda wote nikiwa na Sajuki? Mbona hakuibuka wakati mume wangu akiwa hai? Najua anatumia kigezo cha kuondoka Sajuki kunionea lakini Mungu anajua.”

NI KWELI ALIFUNGA NDOA NA KUSHI?
Pamoja na kumbembeleza aeleze kama kweli aliwahi kufunga ndoa na Kushi, Wastara alisema: “Sitaki kumzungumzia mtu, naomba watu wawe na huruma kwangu, wasitumie kigezo cha kumpoteza Sajuki kunidhalilisha.”

SHEHE AMPINGA KUSHI
Gazeti hili halikuishia hapo, lilimtafuta shehe wa Msikiti wa Nuur wa Magomeni-Mapipa jijini Dar, Juma Simba ili kupata ufafanuzi juu ya talaka moja ambapo alimpinga Kushi kwa kusema kuwa kisheria Wastara si mkewe tena.
“Kumpa talaka moja si sababu ya kuendelea kuwa mke wake mpaka leo hii, sheria inasema kuwa Kushi alitakiwa kumrejea Wastara kabla ya miezi mitatu kupita tangu alipompa talaka moja,” alisema na kusisitiza kuwa ndoa hiyo ilishakufa.

YATOKANAYO
Awali ilidaiwa kuwa Wastara aliwahi kuolewa mara mbili kabla ya kufunga ndoa na staa mwenzake wa filamu, Sajuki.
Ndoa ya kwanza ya Wastara aliifunga mwaka 1998 na Juma Mpemba ambaye alibahatika kupata naye mtoto mmoja wa kiume aitwaye Samir.
Sajuki alikuwa mume wa tatu kwa Wastara ambaye naye alibahatika kupata mtoto mmoja wa kike aitwaye Farheen.

0 comments:

Chapisha Maoni