Alhamisi, Septemba 28, 2017

NYERERE ALIUCHUKULIAJE UKAHABA? ALIAMUA NINI WALIPOFUKUZWA NA RC RWEGASIRA 1980?

 HUENDA ni jambo lisiloingia akilini kwa hali ya kawaida, pale mwenendo uonekanao ni dhambi kwa Mungu, kutetewa na mtu atambuliwaye na wengi ni Mcha-Mungu!
Hata hivyo, kwa mujibu wa kauli ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyejulikana vile, hata ikatabirika baada ya kifo chake kuwa angetangazwa Mwenye Heri hatimaye Mtakatifu, si sahihi mwanadamu kumhukumu mwenziwe isipokuwa Mungu Mwenyewe!
Ndiyo maana ilipopangwa operesheni ya kurejesha makahaba makwao kwa shuruti Dar es Salaam mnamo miaka ya 1980, Mwalimu Nyerere alimuita Ikulu aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo kwa wakati ule, Joseph Rwegasira, akitaka aende akamfafanulie utaratibu na madhumuni ya operesheni ile!
Alipofika, kauli ya kwanza ya Mwalimu ilimtumainisha kuwa huenda operesheni yake iliungwa mkono pale alipohoji, “Nasikia umeamua kuwahamisha mama zangu warudi makwao wakalime maharagwe!” Rwegasira alijibu haraka kwa kusema, “Unajua Mwalimu, hatua yangu hii ni kutekeleza kaulimbiu yetu ya ‘Kilimo ni Uti wa Mgongo wa Taifa Letu’, na operesheni ya ‘Kilimo cha Kufa na Kupona’, pengine hata kaulimbiu ya awali tuliyoita, ‘Siasa ni Kilimo,’ ndipo nikaiona ni muafaka kabisa!”
Hapo ndipo hoja ya Mwalimu iliyofuatia ilimshtua Rwegasira, pale aliposema, “Nimekuita unieleweshe ni watu wa aina gani ulioteua warudishwe makwao kwa utekelezaji huo, pia utaratibu unaotumika!”
Katika mazungumzo yangu na Rwegasira aliniambia ya kuwa angeweza, kuzua aina nyinginezo za watu alioandaa wasafirishwe makwao, lakini kwa jinsi alivyoniamba mwenyewe, ilibidi akiri ya kuwa ilihusu makahaba tu.
Kwani aligundua kwa hisia ya kuwa Mwalimu alikwishakujua hali halisi, hivyo akasema wazi, “Nimedhamiria tu makahaba mheshimiwa, kwa kuzingatia matendo yao!” Ndipo Baba wa Taifa aliishia kuhoji, “Kwa hiyo umewahukumu kwa ukahaba wao, au kuna sababu nyingine?” Hapo, Rwegasira alikaa kimya kwa kutokuwa na jibu muafaka!
Hata hivyo, Baba wa Taifa aliendelea kudadisi kwa kuhoji, “Ikiwa umeamua kuwatimua makahaba, je, mazingira ya kule utakakowahamisha, umeyaandaaje?”
Kwa kuwa hoja ya Baba wa Taifa ilikuja kinyume na matarajio ya Rwegasira, isitoshe hakuelewa mwelekeo wa hoja ile, alibaki kimya, ndipo Mwalimu aliamuamuru kwa kusema, “Ukiweza kutimiza hilo, njoo unieleze nibariki operesheni yako!”
Aliongeza kwa kusema, “Kama usingekuwa mtani wangu wito wangu ungeishia hapa, lakini hebu nikufafanulie chanzo cha ukahaba, ndipo aliuliza iwapo Rwegasira anafahamu wateja wa makahaba ni kina nani, akawa amejibu kuwa ni wanaume!
Mwalimu alicheka akamuuliza, “Wewe si mwanaume, je, huko waliko makahaba unakwenda?” Rwegasira alijibu, “Hapana!” Akahoji tena, “Mimi si mwanaume, je, huko naenda?” Rwegasira alijibu, “Hapana Mwalimu!” Ndipo alianza kumchambulia kuanzia wanaume wasiojua kumtaka mapenzi mwanamke, wasiotaka bughudha ya kutunza familia hivyo hawaoi, hata waliobarikiwa nguvu nyingi za mwili wakienda huko kuzipunguza ili wasisumbue wake zao! Na hapo ndipo Mwalimu alifafanua hoja yake kwa Rwegasira akisema, “Nilipotaka nijue mazingira ya huko utakakowaondoa umeyaandaje, nilijua hao wateja wao wasipowakuta, matokeo ni kubakwa mama zetu, wake zetu, wanafunzi wetu, vilema wetu, hata vichaa wetu! Ndiyo maana katika miji yote duniani makahaba wapo!”
Mwalimu alimalizia kwa kumwambia Rwegasira ya kuwa, hata mataifa yaliyojigamba kuwa na utawala bora na wa sheria, yalishindwa kubuni sheria ya kutawala miili ya watu hususani wanawake hivyo kudhibiti ukahaba, pia michezo hatari kama ndondi na kareti, ikaishia kuhalalisha biashara zinazohusisha ukahaba kwa namna moja au nyingine, tena zikitozwa kodi ya mapato kwa Serikali.
Hatimaye Mwalimu alitaja kuhusishwa kwa ukahaba katika Maandiko Matakatifu, ambapo makahaba hawakuhukumiwa kwa ukahaba wao, isipokuwa walihimizwa wawe na matendo mema, sawa na walivyohimizwa watu wengine!
Alitoa mfano wa kahaba aliyemkimbilia Yesu alipokimbizwa na umati uliotaka wamponde mawe mpaka afe kama mila yao inavyoruhusu. Yesu aliuambia ule umati akisema, “Ikiwa miongoni mwenu kuna asiyepata kutenda mnalomtuhumu nalo, na awe wa kwanza kumtupia jiwe!”
Yesu alishusha macho kuendelea kuchora kielelezo chake, na alipoinua macho sekunde kadhaa baadaye, hakuona mtu hata mmoja! Ndipo alimuamuru kahaba akisema, ‘Inuka uende zako, kawe na matendo mema.’
“Je,” Mwalimu alimhoji Rwegasira akisema, “Kwani Yesu alishindwa kumtamkia kahaba aache ukahaba?” Hapo ndipo Mwalimu alitaja kahaba mwingine aliyemkuta Yesu mahali akifanyiwa karamu akamuangukia akilia, mpaka alimlowesha miguu na kumpangusa kwa nywele zake, akampaka manukato! Yesu alimuambia mwenyeji wake akisema: “Huyu mwanamke amekuzidi, kwa kuniosha miguu kama ilivyo desturi yetu, ambapo wewe hukufanya vile.”
Kwa msingi huu, Mwalimu alimtamkia Balozi Joseph Rwegasira akisema: “Kwa kupewa akili na Mwenyezi Mungu, mwanadamu hatahukumiwa kwa dhambi ya mwenziwe, ndipo kwa hali hiyo, litatimilika agizo la Mwenyezi Mungu kuwa, ‘Usihukumu mwenzio, ndipo nawe hutahukumiwa!’
Maongezi yaliyowezesha kuandikwa makala hii wakati wahusika; Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na Balozi Joseph Rwegasira walishatangulia mbele ya haki, yalifanywa kati yangu (Mtangazaji Mstaafu Florian Kaiza), na Balozi Rwegasira.
Tulikutana jijini Beijing China nilikokuwa kwa kazi ya mkataba katika Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa (CRI), kati ya mwaka 1986 hadi 1993.
Balozi Rwegasira alikuwa katika msafara wa Mwalimu akiwa Mwenyekiti wa Tume ya Ushirikiano wa Nchi za Kusini.
Alikwenda China kuukabidhi uongozi wa nchi hiyo, ripoti ya tume ile baada ya kuvunjwa rasmi mwaka 1992.

0 comments:

Chapisha Maoni