Jumatatu, Mei 29, 2017

MUHUBIRI KATIKA KASHFA YA KUSAMBAZA PICHA ZA NGONO

Polisi nchini Indonesia wamesema mmoja wa wahubiri wa Kiislamu wenye msimamo mkali nchini humo ni mshukiwa katika kisa cha usambazaji wa ujumbe na picha chafu za ngono.
Rizieq Shihab anatuhumiwa kutuma ujumbe wenye maneno mazito ya mahaba na pia picha za utupu alipokuwa anawasiliana na mwanamke mmoja.
Mhubiri huyo, ambaye kwa sasa yupo nchini Saudi Arabia, amekanusha madai hayo.
Bw Rizieq ni kiongozi wa kundi la Islamic Defenders Front (FPI), ambalo liliongoza maandamano makubwa dhidi ya gavana wa zamani wa mji mkuu wa Jakarta Basuki Tjahaja Purnama ambaye alifungwa jela kwa kosa la kuitusi dini ya Kiislamu mwezi uliopita.
Mhubiri huyo ambaye anafahamika sana kwa hotuba na mahubiri yake yenye ujumbe wenye kuzua utata, tayari amefungwa jela mara mbili awali kwa kuzua fujo na kuvuruga amani.
Katika kisa cha sasa, Bw Rizieq anadaiwa kukiuka sheria kali za kukabiliana na uenezaji wa ujumbe, picha au video chafu kwa kutuma ujumbe na picha kwa mwanaharakati Firza Husein, ambaye pia ametajwa kama mshukiwa.

0 comments:

Chapisha Maoni