Ijumaa, Machi 10, 2017

TEMBO HULALA KWA SAA 2 TU!

Utafiti uliotolewa kwenye gazeti la PLoS One la Marekani unasema kwa wastani tembo wa Afrika wanalala kwa saa mbili tu kila siku, na hata baadhi ya siku hawalali kabisa. Tembo wa Afrika ni mamalia wanaolala kwa muda mfupi zaidi.
Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Wits cha Afrika Kusini wamechunguza mwenendo wa kulala wa tembo jike wawili wanaoishi katika hifadhi ya Taifa ya Chobe nchini Botswana kwa kuweka vyombo vidogo vya elektroniki kwenye mikonga yao na vyombo vya GPS kwenye shingo zao.
Baada ya uchunguzi wa siku 35, watafiti wamegundua kuwa kwa wastani tembo hao wanalala kwa saa mbili tu kila siku, na baadhi ya siku hawalali kwa saa 46 mfululizo na kutembea kwa umbali wa kilomita 30. Watafiti wanafikiri huenda hawalali ili kujilinda na simba au wawindaji haramu.
Muda mfupi wa kulala huenda unahusiana na ukubwa wao. Mamalia wakubwa zaidi wanalala kwa muda mfupi zaidi. Kwa mfano, farasi wanalala kwa saa 3 tu kila siku, na mamalia wadogo wakiwemo popo wa rangi ya kahawia, possum na armadilo wanalala karibu saa 20 kwa siku.
Kwa mujibu wa uchunguzi, macho ya tembo yanazunguka kwa kasi wakati wanapolala kila baada ya siku 3 na 4. Wanasayansi wanasema kuzunguka kwa macho wakati wa kulala kunahusiana na ndoto na kuimarisha kumbukumbu. Hali hii haitokei mara kwa mara kwa tembo, lakini tembo bado wana uwezo mkubwa wa kukumbuka.

0 comments:

Chapisha Maoni