Jumamosi, Machi 11, 2017

SERENGETI BOYS KAMBINI KESHO

KIKOSI cha vijana cha timu ya taifa ya Tanzania chini ya miaka 17, Serengeti Boys, kinatarajiwa kuingia kambini kesho Jumapili kwa ajili ya maandalizi ya fainali za michuano ya vijana zinazotarajiwa kuanza Mei 14, mwaka huu nchini Gabon.
Serengeti imepangwa Kundi B ikiwa na mabingwa watetezi wa kombe hilo, Mali pamoja na Niger na Angola ambapo watahitajika kushinda michezo miwili ili kufuzu katika fainali za Kombe la Dunia kwa Vijana zitakazofanyika hapo baadaye nchini India.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas amesema: “Baada ya mapumziko mafupi waliyopewa vijana wa Serengeti Boys, Machi 12, mwaka huu (kesho Jumapili) wataingia kambini hapa Karume kwa ajili ya kuanza maandalizi na watakaa kwa siku 14 na baadaye watakwenda sehemu mbalimbali kucheza mechi za kirafiki.”
Wakati huohuo, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga, keshokutwa Jumatatu anatarajia kutangaza kikosi chake kwa ajili ya mechi za kimataifa za kirafiki zilizopo kwenye Kalenda ya FIFA.

0 comments:

Chapisha Maoni