Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambaye yupo mapumzikoni nyumbani kwake Lubambangwe katika kijijini cha Mlimani, Wilaya ya Chato Mkoani Geita, kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe kuwa Rais, ameungana na waumini wenzake wa Kanisa la Bikira Maria Parokia ya Chato, kusali ibada ya Jumapili ya Pili ya Pasaka ambapo pamoja na mambo mengine amewahusia watanzania wote kuendelea kuliombea Taifa ili liendelee kuwa na amani.
"Niwaombe watanzania wote tuendelee kushirikiana na kushikamana, kwa umoja wetu na siku zote tumtangilize Mungu mbele. Wakati tunaadhimisha wiki moja baada ya kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo, Yesu Kristo alikufa kwa sababu ya dhambi zetu, sisi wote tujitahidi kufuata matendo ya Yesu Kristo ya kusameheana, kupendana, kushirikiana na tusibaguane" Amebainisha Rais Magufuli.
Pamoja na Rais Magufuli na Mkewe Mama Janeth Magufuli, ibada hiyo imehudhuriwa na Waziri Mkuu Mstaafu wa Kenya Mheshimiwa Raila Amoro Odinga na Mkewe Mama Ida Odinga, ambao ni familia rafiki wa Rais Magufuli, waliowasili hapa Chato jana jioni Tarehe 02 April, 2016 kwa mapumziko wakitokea Nairobi, Kenya.
Katika salamu zake kwa waumini wa Parokia ya Chato, Mheshimiwa Odinga amewashukuru watanzania kwa uhusiano mzuri walionao na wakenya, huku akitoa mfano wa jinsi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alivyojitoa kupigania uhuru wa mataifa mengi ya Afrika ikiwemo Kenya.
Mheshimiwa Odinga ametoa mfano wake mwenyewe kuwa Mwalimu Nyerere alimpatia pasi ya kusafiria ya Tanzania, aliyoitumia kwa miaka mitatu kwa ajili ya kwenda kusoma nje ya nchi, baada ya utawala wa Kikoloni wa Kenya kukataa kumpa pasi hiyo.
Kuhusu urafiki wake na Rais Magufuli, Mheshimiwa Odinga amesema urafiki huo ulianza tangu Rais Magufuli alipoteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi na yeye kuwa Waziri mwenye dhamana ya ujenzi wa Kenya, ambapo mara kadhaa walibadilishana uzoefu na kushirikiana katika mipango ya miradi ya ujenzi wa barabara, na kwa umuhimu huo ametoa wito kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuendeleza ushirikiano na mshikamano ulioasisiwa na waasisi Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania, Jalamogi Odinga wa Kenya na Milton Obote wa Uganda.
0 comments:
Chapisha Maoni