Alhamisi, Machi 24, 2016

WAZIRI MAGHEMBE AMEMSIMAMISHA KAZI MTENDAJI MKUU WA HUDUMA ZA MISITU TANZANIA ( TFS), WAKURUGENZI WATATU PAMOJA NA WAKUU WA KANDA NCHI NZIMA

Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof.Jumanne Mghembe amemsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu nchini, (TFS) Bw. Juma Mgoo pamoja na Wakurugenzi wawili wa wakala hiyo ili kupisha uchunguzi kutokana na ukusanyaji usioridhisha wa mapato yatokanayo na mazao ya misitu.
Prof. Maghembe ametaja majina ya Wakurugenzi hao aliowasimamisha kazi kuwa ni Mkurugenzi Rasilimali Misitu, Bw. Zawadi Mbwambo pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi endelevu ya Misitu, Bw. Nurdin Chamuya
Wengine waliosimamishwa kazi ni wakuu wa Kanda za Wakala wa Huduma za Misitu nchi nzima ambao ni Bw. Hubert Haule wa Kanda ya Kusini, Bw. Bakari Rashidi wa kanda ya Mashariki, Bw. Shabani Mwinyi Juma wa kanda ya kati , Emanuel Minja wa kanda ya Magharibi pamoja na Bw. Bruno wa nyanda za juu kusini
Akizungumza leo na Waandishi wa Habari Makao Makuu ya Wizara hiyo jijini Dar es Salaam, Prof. Maghembe amesema hatua hiyo imekuja baada ya kubaini shehena kubwa za magogo aina ya mninga katika Mkoa wa Rukwa wilayani Kalambo yakiwa yamekatwa na kuwekwa ndani ya makontena kule kule ndani ya msitu pamoja na kutengenezewa nyaraka feki zinazoonesha magogo hayo yanatoka nchini Zambia tayari kwa kusafirishwa kupelekwa nchini China lakini hata hivyo baada ya kubaini wizi huo hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa na Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania ( TFS).
Amesema kuwa baada ya kubaini hivyo usiku wa jana aliweza kupata taarifa kuwa shehena ya Magogo hayo yenye thamani ya shilingi milioni 500 yaliyotakiwa kupelekwa Makao makuu ya Wilaya ya Kalambo yamemwagiwa petrol na yamechomwa moto
Aliongeza kuwa kumekuwa na ubadhilifu unaofanywa na Maofisa wa ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali yanayotokana na rasilimali za misitu katika Mikoa na Wilaya kwa kutowasilishwa katika mfuko Mkuu wa Serikali.
Kwa upande mwingine , Prof Maghembe amesema kuwa pesa zitokanazo na makusanyo hayo zimekuwa hazipelekwi benki kwa wakati na hata zikipelekwa benki zimekuwa zikipelekwa pungufu na muda mwingine pesa hizo zimekuwa hazipelekwi kabisa.
Wakati huo huo, Waziri Maghembe amemsimamisha kazi Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Wanyamapori wa Matumizi Endelevu, Dkt. Charles Mulokozi kwa kosa la kukaidi agizo la kusaini vibali vya kusafirisha Wanyamapori nje ya nchi.
Hatua hiyo imekuja baada ya jana nyani 61 kukamatwa katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro na kubaini kuwa Idara ya Wanyamapori ndio iliyotoa vibali vya kusafirisha nyani hao na vibali hivyo vikiwa vimetiwa saini na Mkurugenzi huyo.
Ameongeza kuwa ndege ya kutoka Ulaya Kusini iliyotakiwa kusafirisha nyani hao imeshikiliwa pamoja na rubani wake kwa mahojiano zaidi.
Prof ,Maghembe amesema kutokana taarifa alizozipata kuwa jumla ya nyani 450 ndio waliokuwa wanawindwa kwa ajili ya kusafirishwa kupelekwa nje.

0 comments:

Chapisha Maoni