Raia kumi wa Kenya wameituhumu
Serikali ya Tanzania, kwa kuwateka jijini Maputo nchini Msumbiji Januari
2006, ambako walikuwa wakiishi kihalali wakitafuta fursa za biashara,
na kisha kuwapakiza kwenye ndege ya kijeshi na kuwaleta nchini Tanzania
kwa nguvu.
Kwa upande wake, serikali ya Tanzania kupitia mawakili
wake imepinga madai hayo na kuitaka Mahakama ya Afrika ya Haki za Watu
kutupilia mbali maombi ya watuhumiwa.
Tanzania inasema watuhumiwa
hao walikamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere
baada ya kuletwa kupitia ndege ya jeshi la Msumbiji.
Wakenya hao wanahoji kuwa kesi yao nchini Tanzania imechukua muda mrefu kwa kuahirishwa mara kwa mara bila sababu.
Aidha wanadai kuwa kesi imeendeshwa bila wao kuwa na mawakili wa kuwatetea.
Mawakili
wa serikali ya Tanzania pia waliieleza Mahakama ya Afrika kuwa, wawili
kati ya raia hao wa Kenya waliofariki wakiwa magereza, walikufa kwa kifo
cha kawaida, na kesi iliahirishwa mara kwa mara kutokana na mawakili wa
walalamishi kukosa kufika mahakamani siku za kesi.
Wakenya hao
walikamatwa miaka kumi iliyopita na kuhukumia kufungwa miaka thelathini
jela, baada ya kukutwa na hatia ya kosa la mauaji na ujambazi wa kutumia
silaha lililofanyika katika benki ya NMB Tawi la Moshi, mwezi Mei 2004.
Mahakama
ya Africa kuhusu haki za binadamu na za watu iliundwa mwaka 2006 na
kuanza kazi zake rasmi mwaka mmoja baadaye. Hadi kufikia mwishoni mwa
mwezi februari 2016, Mahakama imepokea kesi 74, ambapo 25 kati ya hizo
zimekwisha shughulikiwa, huku kesi 4 zikipelekwa katika Tume ya Afrika
ya Watu na Haki za Binadamu nchini Gambia.
0 comments:
Chapisha Maoni