Jumatano, Machi 30, 2016

WAFANYAKAZI WATATU WA TANESCO WAMEKAMATWA NA POLISI KUFUATIA KIFO CHA MWENZAO ALIYENASWA NA UMEME JUU YA NGUZO MOROGORO

Wafanyakazi watatu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) mkoani Morogoro, wanashikiliwa na Polisi wakihojiwa kutokana na kifo cha mfanyakazi mwenzao, Deo Elias (30), mkazi wa Mazimbu, Manispaa ya Morogoro kwa kunaswa na umeme juu ya nguzo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 5.30 asubuhi maeneo ya Mafiga, wakati Elias akiwa na wafanyakazi wenzake katika eneo la kazi.
Kamanda Matei alisema Elias alipokuwa na wenzake katika eneo hilo wakirekebisha umeme, alinaswa na kufa papo hapo.
Meneja wa Tanesco Mkoa wa Morogoro, Mhandisi John Bandiye akizungumzia tukio hilo ofisini kwake jana, alisema Elias alikuwa katika kazi za kawaida kama fundi na tukio hilo limetokea kwa bahati mbaya.
Mhandisi Bandiye alisema mfanyakazi huyo alikuwa akirekebisha njia ya umeme ya Ngazengwa iliyopo eneo la Mafiga na ilikuwa imezimwa, lakini cha kushangazwa ilikuwa na umeme uliosababisha kifo chake.
“Kwa sasa shirika lina wafanyakzi wa muda wanaosaidiana na mafundi wakuu na hupatiwa mafunzo na wanatambulika, tofauti na maneno yaliyozagaa mitaani kuwa marehemu hakuwa mfanyakazi,” alisema.
Alisema mwili wake umesafirishwa kwenda kwao mkoani Mbeya kwa ajili ya maziko.
Awali, Fundi wa TANESCO Morogoro, Deo Elias (30) mkazi wa Mazimbu Road ,alifariki dunia kwa kupigwa shoti ya umeme na kuungua wakati akifanya matengenezo ya laini kubwa ya umeme ya 11 KV katika eneo la Mafiga, Manispaa ya Morogoro.

0 comments:

Chapisha Maoni