Ijumaa, Machi 25, 2016

SASA TANZANIA NA SAUDI ARABIA DAMUDAMU

Mfalme wa Saudi Arabia Mtukufu Salman Bin Abdulaziz Al Saud amemhakikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, kuwa nchi yake imeichagua Tanzania kuwa nchi ya kipaumbele katika mpango wake wa kuimarisha zaidi mahusiano na Afrika uliolenga kuendeleza na kukuza biashara, uwekezaji na kushiriki katika miradi ya maendeleo.
Ujumbe wa Mtukufu Salman Bin Abdulaziz Al Saud umewasilishwa kwa Rais Magufuli leo tarehe 24 Machi, 2016 na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Mheshimiwa Adel Al Jubeir Ikulu Jijini Dar es salaam.
Katika Salamu hizo pamoja na kumpongeza Rais Magufuli kwa kuchaguliwa kuiongoza Serikali ya awamu ya tano ya Tanzania, Mfalme Salman Bin Abdulaziz Al Saud amesema Saudia Arabia imedhamiria kukuza zaidi mahusiano kati yake na Tanzania ili kuwaletea manufaa makubwa wananchi.
Kwa upande wake Rais Dkt. John Pombe Magufuli amemshukuru Mfalme wa Saudi Arabia kwa kumtumia ujumbe na kumpongeza kwa kuchaguliwa kuiongoza Tanzania na amemhakikishia kuwa Serikali yake itafurahi kuona Saudi Arabia inashirikiana na Tanzania kutekeleza miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kati na barabara.
Maeneo mengine ambayo Rais Magufuli na Waziri Adel Al Jubeir wameyazungumzia ni ushiriakiano kati ya Tanzania na Saudia Arabia katika kuendeleza Elimu, Utalii, Bandari na miundombinu.
Pamoja na kufanya Mazungumzo hayo, Rais Magufuli pia ameshuhudia utiaji saini wa mkataba kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na Saudi Arabia katika nyanja za Uchumi, Biashara, Uwekezaji, Ufundi, Vijana na Michezo, ambapo kwa upande wa Tanzania mkataba huo umesainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Balozi Augustine Mahiga, na kwa upande wa Saudi Arabia umesainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Mheshimiwa Adel Al Jubeir.

0 comments:

Chapisha Maoni