Rais wa Jamuhuri ya Mungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli
amekabidhi gari la kubebea wagonjwa kwa hosipitali ya wilaya ya
Chalinze, Ikiwa ni utekelezaji wa ilani na ahadi ya uchaguzi ya Chama
Cha Mapinduzi CCM kwa wananchi ikiwa ni pamoja na wa jimbo la Chalinze.
Gari hilo la kubebea wagonjwa limekabidhiwa kwa niaba ya Rais, na
Katibu Mkuu Ikulu Peter Ilomo kwa Mbunge wa Jimbo la Chalinze
Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete Ikulu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
mara baada ya kukabidhi gari hilo, Katibu Mkuu Ikulu Ndugu Peter Ilomo
amesema gari hilo limetolewa na Mheshimiwa Rais kwa hosipitali hiyo
ikiwa ni kuitikia wito na utekelezaji wa ilani na ahadi ya uchaguzi ya
Chama Cha Mapinduzi CCM ya kuboresha huduma ya afya kwa wananchi wake
kote nchini. Aidha, Ndugu Ilomo amewaomba viongozi wa jimbo la Chalinze
kulitumia gari hilo kwa matumizi yaliyokusudiwa ya kuwahudumia wananchi
wa eneo hilo.
Akipokea gari
hilo kwa niaba ya wananchi wa jimbo na Wilaya ya Chalinze, Mbunge wa
jimbo la Chalinze Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete amemshukuru Mheshimiwa
Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa msaada huo na kuahidi kulitumia
gari hilo kwa malengo yaliyokusudiwa, na kusema kuwa, utendaji kazi wa
Rais Magufuli umekuwa ukiungwa mkono na wananchi wa kada mbalimbali na
kuwaomba watanzania kuzidi kumuombea kwa Mungu.
Kwa upande wake
Dakta Nasoro Ally Matuzya, amesema gari hilo limekuja kwa wakati muafaka
kwa kuwa umezingatia utekelezaji wa malengo ya Milenia hususan lengo
namba nne linalosisitiza kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto
chini ya miaka mitano
Naye Mwenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya
Chalinze Ndugu Saidi Omar Zikatimu amesema gari hilo la kubebea wagonjwa
litakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa jimbo hilo la Chalinze hususan
katika kusaidia kutoa wagonjwa ambao wako katika maeneo ya vijijini
wilayani humo na kuwafikisha katika hospitali ya Chalinze na hivyo
kunusuru maisha yao kwa kupata huduma za afya kwa haraka.
Mbali
na Wilaya ya Chalinze kupata msaada wa gari hilo la kubebea wagonjwa,
tayari magari mengine mawili ya kubebea wagonjwa yameshakabidhiwa katika
vituo vya afya vya Kiroka na Kisemu mkoani Morogoro.
Hospitali
mpya ya Wilaya ya Chalinze imepanda hadhi kutoka kituo cha Msoga ambayo
ilikuwa haina gari la kubebea wagonjwa na hivyo kufanya usafirishaji wa
wagonjwa kutoka hospitali hiyo hadi hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Pwani
ya Tumbi au kutoka maeneo ya vijijini kuwa mgumu.
0 comments:
Chapisha Maoni