Jumatatu, Machi 21, 2016

MWANAMKE ALIYEKUWA NA WANAUME WAWILI GUEST HOUSE WAMEUAWA MBEYA

Watu watatu wamefariki dunia kwa kunyongwa na miili yao kuchomwa moto ndani ya nyumba ya wageni iliyopo Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya.
Mauaji hayo yamegubikwa na utata kutokana na mazingira ya tukio hilo kuwahusisha wapangaji wa nyumba hiyo usiku wa kuamkia jana.
Mmiliki wa nyumba hiyo iliyopo Mtaa wa Kyela Kati, Boniface Mtengela alisema waliouawa ni watatu kati ya watu wanne waliofika kwa pamoja saa nne usiku siku ya juzi
Alisema watu hao walikuwa wanaume watatu na mwanamke mmoja na waliouawa ni mwanamke na wanaume wawili.
Mtengela alisema wanaume wawili walijiandikisha kwa jina la Ali Hassan na mwanamke la Mariam.
“Mwanamume mmoja alipanga chumba namba 14, mwingine 105 na mwenye mke alipanga chumba namba 15. 
"Waliokutwa wamekufa ni wanaume wawili wa vyumba na 14 na 105 pamoja na mwanamke huku mwanamume mwenye mke akitoroka,”alisema.
Mganga Mfawidhi wa Wilaya ya Kyela, Francis Mhagama alisema uchunguzi wa miili ya marehemu hao umebaini kuwa waliuawa kwa kunyongwa kisha kuchomwa moto baada ya kumwagiwa mafuta ya taa.
Uchunguzi katika eneo la tukio ulibaini miili yao iliungua, lakini chumba na magodoro havikuungua. Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Kyela Kati, Timoth Luvanda alisema usiku wa tukio hilo hakusikika kelele zozote.
Kamanda wa polisi mkoani Mbeya, Ahmed Msangi hakupatikana kuzungumzia tukio hilo wala kukamatwa kwa mmiliki wa nyumba hiyo na kuhojiwa katika Kituo cha Polisi Wilaya ya Kyela.

0 comments:

Chapisha Maoni