Jumatano, Machi 23, 2016

MUENDELEZO WA TAARIFA YA MWANAMKE ALIYEKUTWA NA MAUTI GUEST HOUSE PAMOJA NA WANAUME WAWILI KYELA, MBEYA

HATIMAYE maiti za watu watatu waliouawa kikatili baada ya kunyongwa na miili yao kuchomwa moto ndani ya chumba kimoja zimetambuliwa, wamo ndugu wa familia moja.
Wakati taarifa ya jeshi la polisi iliyotolewa juzi na Kamanda wa polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi,ikiwataja marehemu hao kuwa ni Mariam Hassan, Abbas yasini na Tatizo Adamu wote wakazi wa Songea, Mkoani Ruvuma.
Hata hivyo, baada ya ndugu hao wa marehemu kuwatambua, wametaja majina halisi ya marehemu hao na kusema kuwa si wakazi wa Songea, bali wote ni wakazi wa miji ya Ilomba na Mbarali, Mkoani Mbeya na kwamba si wafanyabiashara.
Akizungumza kwa niaba ya familia, Riziki Chaula,
aliyejitambulisha kuwa ni kaka wa marehemu wawili, aliwataja marehemu hao kuwa ni Zauda Omar (34) , Mkazi wa Ilomba, Jijini Mbeya na Baraka Chaula (28) Mkazi wa kijiji cha Utulo kata ya Mapogolo, Wilayani Mbarali ambapo ni ndugu.
Alimtaja marehemu watatu kuwa ni Rodgers Simwaka, Mkazi wa Ilomba, Jijini Mbeya na kwamba ni jirani wa marehemu Zauda na amekuwa akijihusisha na shughuli za kusajili laini za simu katika maeneo mbalimbali Mkoani humo.
Aliongeza kuwa, mbali na marehemu Zauda kuwa ni mdogo wake waliochangia baba, lakini pia alikuwa ni mke wa mtu na hadi mauti inamfika walikuwa wakiishi kwa amani na mumewe aliyemtaja kwa jina la Abdalah Malifyuma.
“Vifo hivi vimetuacha kwenye mkanganyiko mkubwa sana…..kwani Zauda na Baraka ni dada na kaka mtu na huyo mwingine ni jirani yao, sasa iweje watoke Mbeya hadi Kyela na kukutwa wakiwa wamenyongwa ndani ya chumba kimoja” alihoji Riziki.
Aidha, Riziki aliongeza kuwa, siku moja kabla ya tukio marehemu Zaudi alikuwa amewasiliana na majirani zake, pamoja na mumewe na kuwaaga kuwa alikuwa na safari ya kwenda na kurudi Wilayani Rungwe.
Majirani wasimulia.
Hata hivyo, licha ya majirani wa marehemu Zauda kusimulia jinsi walimfahamu marehemu na kuishi naye, lakini mume wa marehemu huyo alikataa kuzungumza chochote juu ya tukio hilo la mauaji, huku muda wote akionekana kulia kwa hisia kali.
Mmoja wa majirani wa marehemu Zauda, Said Nkenja alisema siku moja kabla ya tukio marehemu aliaga kuwa angesafiri kwenda kwenye shughuli zake Mjini Tukuyu, Wilayani Rungwe na kwamba taarifa za kuuawa kwake zimewashitua na kuzua hofu kubwa.
Kwa upande wake, rafiki wa karibu na marehemu Rodgers, aliyejitambulisha kwa jina la Sebastian Aman, alisema siku mbili kabla ya tukio la kuuawa kikatili kwa rafiki yake ambaye walikuwa wakifanya kazi ya kuuza laini za simu, alimuaga kuwa alikwa na safari kikazi ya siku tatu ya kwenda Wilayani Chunya.
Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Wilaya ya Kyela, Dk.Frencis Mhagama, alithibitisha miili ya marehemu hao kutambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao baada ya kukaa hospitalini hapo kwa siku.

1 comments:

  1. Dunia sijaelewa inaenda wapi na tatizo ni nini watu watatu kuuwawa kwa pamoja katika chumba kimoja aisee binadamu tumekuwa wakatili sana, Lakini sara na maombi ya Mungu wa kweli Yehova yanahitajika kwa kiasi kikubwa sana...

    JibuFuta