ZIKIWA zimebaki siku nne, kwa wanafunzi wa shule ya sekondari ya wavulana ya Iyunga, kurejea shuleni kuendelea na masomo baada ya kufungwa kwa wiki tatu kufuatia ajali ya moto ulioteketeza mabweni na mali za wanafunzi 151, bado hali imeonekana kuwa tete baada ya baraza la madiwani la Halmashauri ya Jiji la Mbeya, kuendelea kugoma kupitisha maombi ya shilingi milioni 235.
Madiwani hao, wamekuwa wakihoji uhalali wa kiasi hicho cha fedha, kilichoombwa na halmashauri ya Jiji la Mbeya kwa ajili ya kuanza kwa ukarabati wa mabweni, utengenezaji wa vitanda na ununuzi wa vifaa mbalimbali kwa wanafunzi 151, ikiwa baadhi ya wadau mbalimbali wamewasilisha michango yao ambayo thamani yake haijahainishwa na wala taarifa ya mapato na matumizi haijawasilishwa kwa kamati husika .
Mbali na hilo, pia kamati ya fedha ilipoketi mapema mwezi huu, ilishindwa kufikia muafaka wa kupitisha matumizi hayo ya fedha na kuwataka wataalamu wa idara husika kuhakikisha wanaainisha vitu vyote vilivyopokelewa kama msaada ikiwa na kufahamu thamani yake, ili kufahamu ni kiasi gani halali kinachohitajika kutolewa na halmashauri hiyo.
Pia, wajumbe hao wamelalamika kutoshirikishwa kwenye mambo mengi yanayoihusu dharura hiyo ya ukarabati wa shule ya Iyunga, kufuatia ajali hiyo ya moto huku wakitolea mfano, harambee ya kwanza iliyodaiwa kuitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Munasa Nyirembe kwa madai kuwa ilikuwa si halali kwani mpaka sasa taarifa zake za fedha zimekuwa zikighubikwa na utata.
0 comments:
Chapisha Maoni