Ijumaa, Februari 12, 2016

VIDEO; SIKU 100 ZA RAIS MAGUFULI

LEO ni siku ya 100 tangu Rais John Magufuli alipoingia Ikulu ya Magogoni, Dar es Salaam, na tangu alipotoa hotuba yake siku ya kuapishwa na ile ya uzinduzi wa Bunge la 11, ameishi katika maneno yake kwa kutenda kile anachokisema.
Miongoni mwa mambo aliyoahidi ni kupambana na rushwa pamoja janga la dawa za kulevya, akisema dawa za kulevya zimeathiri vijana wengi, hivyo akaahidi kushughulikia mtandao huo na wakubwa wanaohusika. Kwa upande wa rushwa, Rais Magufuli aliahidi kupambana na ufisadi na rushwa na katika kutekeleza hilo, alisema ataunda mahakama maalumu ya kushughulikia wezi wakubwa yaani mafisadi. Pia aliahidi kuwashughulikia wafanyakazi wazembe ili serikali yake isiendelee kulea watu wanaolipwa mishahara tu wakati hawafanyi kazi yoyote.
Katika kubana matumizi ya serikali, aliahidi kudhibiti warsha ambazo hazina umuhimu katika serikali wala kuongeza ufanisi kwa wafanyakazi. Aliahidi pia kudhibiti safari za nje, ambazo zimekuwa zikigharimu Serikali fedha nyingi ambazo zingeweza kutumika katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo. Rais Magufuli pia alisema Serikali yake itaongeza wigo katika ukusanyaji wa mapato, ukizingatia kuwa kodi ni kitu muhimu na ni lazima zikusanywe.
Aliahidi kufufua viwanda viliyobinafsishwa, ambavyo baadhi alidai vimegeuzwa mazizi ya mbuzi wakati waliopewa kwa madhumuni ya kuviendeleza. Aliahidi pia kushughulika na kero zinazolalamikiwa kutendwa na polisi, hospitali, mizani, mahakama, maliasili na vilio vya wachimbaji. “Inabidi haya yote niyataje ili nijue tunaanzia wapi na tunakwenda wapi, nisipoyataja nitakuwa mnafiki,” alisema Rais Magufuli wakati akizindua Bunge la 11 mjini Dodoma.
Tayari Rais Magufuli ametenda yale ambayo aliyaahidi kwa Watanzania. Amebana matumizi ya serikali kwa kudhibiti safari zisizo na tija, matumizi yasiyo ya lazima, ameshughulikia watumishi wazembe, ameshughulikia mafisadi ndani ya serikali na kutoa elimu ya bure. Alivyoanza kazi mara tu baada ya kuingia ofisini, alimwapisha Mwanasheria Mkuu, George Masaju aliyemteua muda mfupi tu baada ya kuapishwa.
Kesho yake, rais alifanya ziara ya kushtukiza katika Wizara ya Fedha ambako aliagiza maofisa wa wizara hiyo, kuhakikisha wanaongeza kasi ya ukusanyaji mapato kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), hususani kwa wafanyabiashara wakubwa bila kuogopa. Rais alionekana tofauti na viongozi wengine waliomtangulia baada ya kuifanya sherehe ya kuzindua Bunge kutokuwa ya kifahari na hivyo akaokoa Sh milioni 251, ambazo aliagiza zikanunue vitanda Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Jumla ya vitanda 300, magodoro 300, viti maalumu vya wagonjwa 30, vitanda vya kubeba wagonjwa 30 na mashuka 1,695 vilinunuliwa kwa ajili ya Hospitali ya Muhimbili. Rais Magufuli pia alifuta gwaride la Siku ya Uhuru, badala yake akaamuru siku hiyo iadhimishwe na wananchi wote kwa kufanya usafi maeneo yanayowazunguka ili kudhibiti ugonjwa wa kipindupindu.
Wananchi waliitikia agizo hilo kwa wingi na kufanya usafi mkubwa. Fedha Sh bilioni nne zilizopaswa kutumika kugharimia shamrashamra za Siku ya Uhuru, ambazo zingefanyika tarehe 9 Desemba 2015, Rais aliamuru zitumike kufanya upanuzi wa barabara ya Mwenge hadi Morocco jijini Dar es Salaam yenye urefu wa kilometa 4.3, kwa kuongeza njia mbili za barabara za lami.  Ujenzi wa barabara hiyo tayari umeanza.

Rais alianza kazi ya kutumbua majipu siku yake ya nne akiwa ofisini, alifanya ziara ya ghafla katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ambako alijionea huduma zilizozorota hospitalini hapo na hivyo akalazimika kuivunja Bodi ya Wakurugenzi ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) pamoja na kumuondoa madarakani Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Hussein Kidanto.
Baadaye Waziri MKuu Kassim Majaliwa alifanya ziara katika Bandari ya Dar es Salaam, ambako aligundua upotevu wa makontena 329. Hatua iliyosababisha rais kumsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade na kumteua Dk Phillip Mpango kukaimu nafasi hiyo. Kabla ya Bade, Majaliwa alishatangaza kuwasimamisha kazi Kamishna wa Forodha, Tiagi Masamaki na Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Wateja, Habibu Mponezya.
Wengine waliokumbwa na ufagio huo ni Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Haruni Mpande, Hamisi Ali Omari na Mkuu wa Kitengo cha Bandari Kavu, Eliachi Mrema. Majaliwa pia aliagiza watumishi watatu wa mamlaka hiyo, wahamishwe kutoka Dar es Salaam na kupelekwa mikoani, ambao ni Anangisye Mtafya, Nsajigwa Mwandengele na Robert Nyoni, lakini baadaye akabadilisha uamuzi wake na kuamuru watumishi hao nao wasimamishwe kazi.
Upotevu huo wa makontena pia ulisababisha TRA kuwasimamisha kazi watumishi wake 35 na kampuni 43 za uwakala wa forodha, zilisimamishwa kwa tuhuma za kuhusika kutorosha makontena hayo. Uchukuzi, Bandari na Reli Baada ya kubainika matumizi ya Sh bilioni 13 za Kampuni ya Reli (TRL) kutumika kiholela, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaaban Mwinjaka kwa ajili ya kupisha uchunguzi dhidi ya matumizi mabaya ya fedha hizo.
Pia Rais Magufuli siku hiyo aliivunja Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), iliyokuwa chini ya Profesa Joseph Msambichaka kutokana na kubainika madudu mengi bandarini hapo. Rais pia alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Awadh Massawe. Takukuru Katika kutimiza ahadi yake ya kupambana na ufisadi, Rais Magufuli pia alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kudhibiti Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hosea.
Alimteua pia Naibu Mkurugenzi Valentino Mlowola kukaimu nafasi hiyo. RAHCO Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO), Benhadard Tito naye alisimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi wa kina kutokana na ukiukwaji mkubwa wa taratibu za manunuzi, uliobainika katika mchakato wa utoaji wa zabuni ya ujenzi wa Reli ya Kati. Licha ya kusimamishwa kazi kwa Mkurugenzi Mkuu wa Rahco, Rais Magufuli pia aliivunja Bodi ya Rahco.
Vitambulisho vya Taifa Kutokana na malalamiko ya kusuasua kwa utoaji wa vitambulisho vya Taifa, Rais pia alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu na kuwasimamisha kazi maofisa wengine wanne wa taasisi hiyo.
Maofisa wanne wa NIDA waliosimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi wa namna Sh bilioni 180 zilivyotumiwa na mamlaka hiyo wakati wananchi waliopatiwa vitambulisho vya taifa na mamlaka hiyo ni wachache ni Mkurugenzi wa Tehama, Joseph Makani, Ofisa Ugavi Mkuu, Rahel Mapande, Mkurugenzi wa Sheria, Sabrina Nyoni na George Ntalima ambaye ni Ofisa Usafirishaji.
Rais pia aliiagiza Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa kuwarejesha nyumbani mara moja mabalozi wawili, ambao mikataba yao iliisha. Mabalozi hao ni Batilda Buriani aliyeko Tokyo nchini Japan na Dk James Msekela aliyeko Rome, Italia. Rais alimrejesha nyumbani Balozi wa Tanzania aliyeko London, Uingereza, Peter Kallaghe.
Balozi huyo anarejea wizarani ambako atapangiwa kazi nyingine. Uhamiaji Madai ya kukithiri kwa rushwa katika Idara ya Uhamiaji pia kulimfanya Rais Magufuli kumsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, Sylvester Ambokile na Kamishna wa Uhamiaji anayeshughulikia Utawala na Fedha, Piniel Mgonja ili kupisha uchunguzi katika idara hiyo nyeti nchini.

Katika siku zake 100 akiwa Ikulu, Rais Magufuli ametenga Sh bilioni 137 kwa ajili ya kugharimia utoaji wa elimu ya bure kuanzia Januari hadi Juni mwakani. Elimu bure inatolewa kuanzia shule ya awali hadi kidato cha nne.

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, ametoa taarifa ya siku 100 za kwanza za Serikali ya awamu ya tano Ikulu jijini Dar es salaam leo Ijumaa Februari 12, 2016.

Tazama video hapa chini.

0 comments:

Chapisha Maoni