Ugonjwa wa homa ya Lassa umeendelea kuenea ambapo sasa umefika nchini Benin. Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Benin, watu 12 tayari wamethibitika kukumbwa na homa hiyo nchini humo kuanzia mwezi Januari hadi sasa.
Wizara ya Afya ya Benin sanjari na kuthibitisha habari hiyo, imesema kuwa watu wanne miongoni mwa waathirika hao ni wafanyakazi wa sekta ya huduma ya afya ya nchi hiyo. Hii ni katika hali ambayo serikali ya Nigeria hivi karibuni ilitangaza kuwa watu 101 wamekwishapoteza maisha yao kutokana na homa hiyo. Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na kituo cha kudhibiti na kuzuia magonjwa cha Marekani, idadi ya watu wanaokumbwa kila mwaka na homa ya Lassa huko magharibi mwa Afrika huwa ni kati ya watu laki moja hadi tatu, huku idadi ya watu wanaopoteza maisha ikiwa ni karibu watu elfu tano. Virusi vya homa ya Lassa huambukiza kupitia chakula, kugusa vyombo au kitu chenye unyevunyevu wenye virusi hivyo au kugusa mwili wa mtu mwenye maradhi hayo.
0 comments:
Chapisha Maoni