Jumatano, Februari 03, 2016

UGONJWA WA HOMA YA ZIKA BADO HAUJAINGIA NCHINI TANZANIA

Kumekuwepo na taarifa kupitia vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa kuhusu ugonjwa wa Homa ya Zika ambao unasababishwa na kirusi kijulikanacho kama "Zika Virus".
Ugonjwa huu unaenezwa na mbu aina ya Aedes ambae huwa ana tabia ya kuuma asubuhi na pia nyakati za mchana/jioni. Kirusi cha Homa ya Zika kama kile cha Dengue kinaambukizwa kutoka mtu mmoja hadi mwingine kwa kuumwa na mbu wa jamii ya Aedes hasa Aedea aegypti.
Serikali kupitia Wizara ya Afya imefanya ufuatiliaji wa ugonjwa huu katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini pamoja na mipakani kupitia mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa wa Wizara (surveillance health system).
Tumejiridhisha kuwa ugonjwa wa homa ya Zika kwa sasa bado haujaingia nchini. Hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi ila waendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu pamoja na magonjwa ya Dengue na Malaria kwa ujumla kwa kujikinga na kuumwa na mbu.
Tunaendelea kuwasiliana kwa karibu na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa lengo la kupata Taarifa na Maelezo zaidi ya kukabiliana na ugonjwa huu. Kamati ya Dharura ya Miongozo ya Kimataifa ya Afya ya WHO yaani International Health Regulations Emergency Committee" itakutana kesho Jumatatu tare 1 Feb mjini Geneva Uswisi ili kufanya tathmini ya ugonjwa huu na kutoa Tamko/Maelekezo zaidi ya namna ya kuuthibiti ugonjwa wa Zika.
Baada ya Mwongozo huo wa WHO, Wizara ya Afya itaandaa Taarifa ya Tahadhati ya ugonjwa huu kwa ajili ya kusambazwa kwa Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya Tanzania Bara. Taarifa hii itajumuisha namna mgonjwa anavyoweza kutambuliwa (ainisho la ugonjwa), Ukweli kuhusu Ugonjwa (Fact Sheet), Mwongozo kwa watumishi wa agya wa namna ya kuchukua sampuli. Vipepetushi vinavyoelezea jinsi ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huu vitatolewa.
Maelezo zaidi kuhusu Zika Virus yanapatikana katika Taarifa kwa Wananchi na Vyombo vya Habari kuhusu Ugonjwa wa Homa ya Zika (Zika Virus) iliyotolewa na Wizara leo tar 31 Januari 2016

0 comments:

Chapisha Maoni