Jumamosi, Februari 13, 2016

TRA YAFUNGA MGODI WA ALMASI SHINYANGA

Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) mkoani Shinyanga imeufunga mgodi wa uchimbaji wa almasi wa Elly Hilali ulioko Mwadui Shinyanga kwa muda usiojulikana kwa kosa la kushindwa kulipa deni la mapato ya serikali zaidi ya shilingi milioni mia tatu sabini na nne na laki tisa na sabini huku wafanyakazi wa mgodi huo wakilalamika kuathiriwa na kitendo hicho.
Akizungumza kuhusu sakata la kufunga mgodi huo wakala wa ukusanyaji mapato wa TRA Bw.Lyasuka Ibrahim amedai TRA imelazimika kuufunga mgodi wa almasi wa Elly Hilali hadi kiasi cha deni linalodaiwa litakapolipwa huku akidai kuwa uongozi wa mgodi umekaidi amri halali ya kusitisha kazi zote mgodini hapo lakini chakushangaza maofisa ukaguzi wa TRA walipofika katika eneo hilo siku moja baada ya kuufunga mgodi walikuta baadhi ya kazi zikiendelea kama kawaida kinyume na maagizo yao.
Naye kaimu meneja wa kitengo cha uzalishaji katika mgodi huo Bw.Bader Seiph alipoulizwa kwanini amekiuka amri ya kusitisha uzalishaji na kuruhusu magari kuendelea kusomba kifusi chenye madini ya almasi alikataa na kudai hakuna kazi inazoendelea mahali hapo lakini maofisa wa TRA walipofuatilia walikuta magari sita yakiendelea kufanya kazi na kulazimika kuyakamata na kuyapeleka katika yadi ya TRA iliyopo mjini Shinyanga kwa hatua zingine zaidi.
Nao baadhi ya wafanyakazi wa mgodi huo wamelalamika kuhusu kufungwa kwa mgodi na kuuomba uongozi wa mgodi kulipa deni hilo mapema iwezekanavyo kwakuwa hali hiyo itawafanya kuishi maisha ya shida huku meneja wa TRA tawi la Shinyanga Bw.Ernesti Dundee akidai kuwa zoezi la kuwasaka wakwepa kodi ni endelevu hivyo makampuni mengine yalipe kodi ya serikali kabla hayajafikiwa.

0 comments:

Chapisha Maoni