Jumatatu, Februari 01, 2016

TOYOTA KUSITISHA UUNDAJI WA MAGARI YAKE JAPAN

Kampuni kubwa zaidi ya kuunda magari,Toyota, imetangaza kuwa itasitisha uzalishaji wa magari mapya katika viwanda vyake nchini Japan kuanzia Februari 8 kwa sababu ya ukosefu wa vyuma vya kutengenezea viungo vya magari hayo.
Taarifa iliyotolewa na Toyota leo (Jumatatu) ilisema kuwa uamuzi huo umeafikiwa baada ya kutokea kwa mlipuko katika kiwanda chake cha kuunda vyuma vya magari kwa jina Aichi Steel Corporation.
Ni mara ya kwanza kwa kampuni hiyo kusitisha uzalishaji wa magari katika viwanda vyake kote nchini Japan tangu tetemeko kubwa la ardhi mwaka wa 2011. "Hii ilani inamaanisha kuwa tutarejelea shughuli zetu za uzalishaji tarehe nane Februari," Toyota ilisema kwenye taarifa yake na kuongeza kuwa viwanda vyake nje ya Japan havitaathiriwa na uamuzi huo
Kampuni ya Toyota huzalisha magari 14,000 kila siku kwenye viwanda vyake nchini Japan. Mwaka uliopita kampuni hiyo iliunda jumla ya magari milioni nne nchini humo. Uamuzi wa kusitishwa kwa muda kwa uzalishaji wa magari hayo nchini Japan unatarajiwa kuathiri lengo la Toyota la kuzalisha magari milioni 4.13 ifikapo mwisho wa mwaka huu.

0 comments:

Chapisha Maoni