Serikali imezipiga marufuku shule zote binafsi za msingi na sekondari kuongeza kiwango cha ada katika mwaka huu wa masomo na kuzitaka shule zote zilizopandisha ada kinyume cha tamko la serikali kusitisha mara moja ongezeko hilo.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ithibati ya Shule, Hadija Mcheka amesema kuwa kufuatia tangazo la serikali la kuzitaka shule binafsi zinazotaka kupandisha ada kuwasilisha maombi yao kwa Kamishna wa Elimu, shule 45 pekee ndizo zilizowasilisha maombi hayo lakini sababu ilizotoa hazikuwa na mashiko.
Alisema kuwa shule nyingine 900 ziliwasilisha maombi ya kuendelea na kiwango cha ada ilichokuwa ikitoza mwaka jana.
Mcheka alieleza kuwa kati ya sababu zilizotolewa na wamiliki wa shule hizo ni pamoja na kuongeza majengo na kuajiri walimu kutoka nje, sababu ambazo Kamishna wa Elimu aliona hazina mashiko kwa kuwa hazimhusu mzazi.
“Mwingine anasema anataka kupandisha ada kwa vile anataka kuajiri walimu kutoka nje ya nchi, hili nalo halimhusu mzazi ndio maana tumewanyima kibali cha kupandisha ada. Sababu zote hizi hazikumridhisha kamishna ndio maana tumewataka watii agizo la Serikali hadi hapo baadaye,” alisema Mcheka.
Akieleza kuhusu mpango wa kuweka ada elekezi, Mcheka alisema kuwa serikali imemuajiri mtaalam mwelekezi atakayefanya kazi ya kubaini gharama za kumsomesha kila mtoto ili kuisaidia serikali kupanga ada elekezi.
0 comments:
Chapisha Maoni