Rais Museveni ametoa matamshi hayo baada ya Umoja wa Ulaya kukosoa jinsi zozei la uchaguzi wa hivi karibuni nchini Uganda lilivyofanyika. Katika taarifa yao waangalizi wa Umoja wa Ulaya walisema kuwa, chama tawala cha Rais Yoweri Museveni cha NRM, kiliharibu mazingira ya uchaguzi kwa kuzua hofu na wasiwasi dhidi ya viongozi wa upinzani na wafuasi wao. Aidha taarifa hiyo ilibainisha kwamba, siku ya kufanyika uchaguzi huo mkuu vituo vingi vya kupigia kura na hasa katika mji mkuu, Kampala, vilifunguliwa kwa kuchelewa. Akijibu matamshi hayo ya Umoja wa Ulaya Rais Museveni amesema hahitaji nasaha wala mahubiri ya Umoja wa Ulaya, kwani hawako sahihi. Tume ya Uchaguzi ya Uganda juzi alasiri ilitangaza kuwa Yoweri Museveni ni Rais Mpya wa nchi hiyo baada ya kushinda zaidi ya asilimia 60.8 huku mpinzani wake mkuu Kizza Besigye akipata asilimia 35.4. Hata hivyo matokeo hayo yamelalamikiwa na wapinzani. Wakati huo huo, mgombea wa FDC Kizza Besigye leo alitiwa tena mbaroni ikiwa ni mara ya nne katika kipindi cha siku nane. Ingrid Turinawe, mmoja wa maafisa wa Chama cha FDC amethibitisha habari ya kutiwa mbaroni Besigye na kubainisha kwamba, vyombo vya usalama vinapaswa kumuachia huru mgombea wao huyo ili apate nafasi ya kukusanya ushadidi unaothibitisha kwamba, uchaguzi uliomrejesha madarakani Rais Museveni ulijaa wizi na udanganyifu.
0 comments:
Chapisha Maoni