Siku tatu baada ya Rais John Magufuli kueleza kuwa yeye si kichaa, si dikteta wala mnyama, Jaji Thomas Mihayo ameungana na mkuu huyo wa nchi akisema hajauona udikteta wake.
Jaji Mihayo alikuwa akifafanua kauli alizotoa Rais Magufuli kwenye kilele cha Siku ya Sheria, wakati alipomuahidi Jaji Mkuu Othman Chande Sh12.3 bilioni za kuendeshea shughuli za mahakama na kumtaka aharakishe kushughulikia kesi za ufisadi ili Serikali iokoe Sh1 trilioni, ambazo kati ya hizo atatoa Sh250 bilioni kwa ajili ya Idara ya Mahakama.
Rais pia alitaka kesi ambazo watuhumiwa wanakamatwa na ushahidi, zifikishwe mahakamani mara moja na kuamuliwa, lakini akataka asichukuliwe kuwa ni dikteta kutokana na maamuzi yake.
“Ninapochukua hatua mimi si mnyama, si dikteta, si shetani. Ni mpole kweli, lakini inafika mahali lazima nifanye (uamuzi). Yanayofanyika serikalini ni mambo ya ajabu sana, nataka kutoa sadaka yangu, inawezekana hata nikifa naweza kuwa rais wa malaika,” alisema.
Kauli hiyo imeibua mjadala miongoni mwa wanasheria wanaodai Rais anaingilia uhuru wa mahakama kwa kutaka uamuzi wa kesi hizo ufanywe kwa utashi wa Serikali, huku baadhi ya hatua kali anazochukua zikielezewa kuwa zina harufu ya udikteta.
Lakini jana, mkuu huyo wa nchi alipata mtetezi wakati Jaji Mihayo alipoongea na waandishi kufafanua kauli hiyo ya Siku ya She ria, akisema Rais dikteta ni yule asiyefuata misingi ya sheria.
“Wanaosema Magufuli ni dikteta hawawajui madikteta. Hakuna kiongozi dikteta Afrika Mashariki isipokuwa Idi Amini tu,” alisema jaji huyo mstaafu ambaye alisema ameamua kutoa ufafanuzi huo baada ya kuona mjadala mkubwa kuhusu kauli hiyo ya Rais na kupata baraka kutoka kwa Jaji Mkuu, Othuman Chande.
Jaji Mihayo, ambaye ni mwenyekiti wa majaji wastaafu, alihoji inawezekanaje kiongozi ambaye mataifa mengine wanatamani akaongoze nchi yao angalau kwa miezi miwili, aonekane kuwa ni dikteta.
“Magufuli anafuata sheria kwa sababu hajafanya jambo lolote ambalo linamfanya awe juu ya sheria. Sijawahi kusikia kasema mfunge huyu au kusema sheria hii isitumike na hii itumike” alisema.
Alisema ni kawaida kwa viongozi wanaokemea uovu kuonekana kama madikteta kwa sababu wanataka kuondoa rushwa.
Kadhalika, Jaji Mihayo alisema anaupenda utendaji kazi wa Magufuli ili wanaokiuka sheria wawajibishwe na walalahoi wapate haki yao.
Magufuli na Mahakama
Kuhusu ahadi yake ya kuipa Idara ya Mahakama Sh12.3 bilioni ili izitumie kwenye shughuli zake na agizo la kuharakisha uamuzi wa kesi 442 ili Serikali iokoe Sh1 trilioni, Jaji Mihayo alisema kitendo hicho hakiingilii uhuru wa mahakama bali ni katika kuhakikisha kesi zinamalizwa kwa wakati na serikali inakusanya mapato ya kutosha.
“Maneno ya Rais ya kuwataka majaji wamalize kesi kwa haraka na kuwaahidi kiasi kile cha fedha, si kuwahonga bali ni motisha na mbinu ya kukusanya mapato,” alisema.
Alisema kauli ya Rais isitafisriwe kuwa ni lazima Serikali ishinde kesi dhidi ya rufaa ya kodi, bali alitaka majaji wafanye kazi zao kwa wepesi zaidi.
Akifafanua kesi za rufaa za kodi, Jaji Mihayo alisema mashauri hayo yatakusanya fedha nyingi kwa hata kama wanaodaiwa watashinda, kisheria ni lazima watoe theluthi ya kodi wanayodaiwa.
Jaji Mihayo pia alisema maneno ya Magufuli yasichukuliwe kuwa yatawavuruga majaji kwa sababu wanafanya kazi yao kwa kufuata kanuni na sheria.
“Uhuru wa mahakama upo ‘guaranteed (umehakikishwa)’ na katika kifungu namba 107 (a) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano.Hata kama Rais akiamrisha vipi, kama ni kitu ambacho ni kinyume na utaratibu, hakiwezi kutekelezwa” alisema.
Kuhusu Magufuli kuwachukulia hatua majaji na mahakimu 502 ambao hawajafikia malengo ya kumaliza kati ya kesi 250 na 260 kwa mwaka, Jaji Mihayo alisema JPM alionyesha kukerwa na ucheleweshaji wa kesi na wala si kuingilia uhuru wa mahakama.
Alisema hata Jaji Mkuu Othman Chande alishachukua hatua kwa kuwataka mahakimu hao watoe maelezo kabla sheria haijachukua mkondo wake.
“Tatizo la ucheleweshaji wa kesi ni kubwa, si dogo kama unavyofikiria ndiyo maana linamkera JPM,” alisema.
Utendaji wa mawaziri, wakuu wa mikoa
Kadhalika Jaji Mihayo pia alizungumzia pia jinsi mawaziri wa JPM wanavyotoa kauli za kuwafukuza kazi au kuwasimamisha watendaji wa Serikali, akisema siasa inatawala kuliko sheria.
Alisema kisheria kiongozi wa Serikali hawezi kusimamishwa kazi au kufukuzwa bila maandishi.
“Watendaji hawatachukuliwa hatua bila kauli ya waziri kuwa katika maandishi, hilo jambo halichukuliwi kijumla tu,” alisema.
Alisema Katibu Mkuu Kiongozi akimsimamisha au kumfukuza mtu kazi, hilo linakuwa limeshafanyiwa kazi kwa kina.
“Vinginevyo, huwezi kumfukuza mtu kazi bila mchakato na uchunguzi wa kuhakiki kama ni kweli ana haki ya kusimamishwa au kufukuzwa,” alisema.
0 comments:
Chapisha Maoni