Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametembelea kwa ghafla wodi ya Wazazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es salaam, na kujionea hali ya msongamano mkubwa wa wazazi uliosababishwa na uhaba wa vitanda na nafasi finyu katika wodi hiyo.
Rais Magufuli aliyekuwa akitoka katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete alikokwenda kumuona na kumjulia hali Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubery Bin Ally, amelazimika kwenda katika wodi hiyo baada ya msafara wake kusimamishwa na kundi la akina mama, waliomtaka kwenda katika wodi ya wazazi ili akajionee jinsi wazazi wanavyokabiliwa na kero mbalimbali ikiwemo ya kulala chini kutokana na kukosa vitanda.
Baada ya kujionea mwenyewe kero ya msongamano na kuzungumza baadhi wazazi waliojifungua, Rais Magufuli amewaahidi wazazi hao kuwa atashughulikia kero alizozishuhudia.
"Nimeiona hali halisi mimi mwenyewe, watu wanapata shida, watu wana mateso, na ndio maana nimeamua kuja kwa makusudi, sikuomba ruhusa ili nijionee hali ilivyo, nimejifunza mengi, ninayabeba na nitajua namna ya kuyatatua" Alisema Rais Magufuli.
Kabla ya kutembelea wodi ya wazazi, Dkt. Magufuli amemjulia hali Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubery Ally aliyelazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ambapo amempa pole na kumuombea apone haraka.
Pamoja na kupokea pole ya Rais, Mufti wa Tanzania ameongoza dua ya kumuombea heri Rais Magufuli ili aweze kutekeleza vyema majukumu yake katika kuwahudumia watanzania.
Dua kama hiyo pia imefanywa na wananchi wengine waliokuwa wakimsubiri nje ya majengo ya Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo katika dua hiyo wamemuomba Mwenyezi Mungu kumlinda na kumuongoza katika majukumu yake ya kuiongoza nchi.
"Mwenyezi Mungu mbariki Rais wetu, mpe hekima, busara na upendo katika kazi zake za kuiongoza nchi hii ili watanzania wote wanufaike" ilisema sehemu ya dua hiyo iliyoongozwa na mmoja wa akina Mama.
0 comments:
Chapisha Maoni