Alhamisi, Februari 11, 2016

A/KUSINI KUMPOKONYA UONGOZI MJUKUU WA MANDELA BAADA YA KUSILIMU

Baraza la Viongozi wa Kitamaduni nchini Afrika Kusini limemtaka Mandla Mandela, mjukuu wa Rais wa kwanza mzalendo wa nchi hiyo, hayati Mzee Nelson Mandela kujiuzulu wadhifa wake wa Mkuu wa kabila la Mvezo, ambalo ni katika jamii ya Waxhosa katika mkoa wa Eastern Cape, baada ya kusilimu na kuoa binti wa Kiislamu.
Mwelo Nonkonyane, Mkuu wa Baraza la Viongozi wa Kitamaduni nchini Afrika Kusini amesema baraza hilo limeghadhabishwa mno na hatua ya Mandla kuikubali dini ya Uislamu na kisha kuoa bila kuwapa taarifa akisisitiza kuwa, walitaraji binti aliyeolewa ndiye angefuata dini ya mumewe na sio kinyume chake. Baraza hilo limesema Mandla amekiuka kanuni na desturi zao za jadi na limemshutumu kuwa ameoa bila kuwashirikisha wazee wa kitamaduni.
Mandla Mandela alifunga ndoa na Rabia Clarke katika msikiti mmoja mjini Cape Town Afrika Kusini mwishoni mwa wiki. Shekh Ibrahim Gabriel aliyeendesha nikaha hiyo katika msikiti wa Kensington siku ya Jumamosi amethibitisha kuwa Mandla alisilimu mwaka uliopita na kuwa ndoa hiyo ilifungwa kwa mujibu wa misingi ya dini ya Kiislamu.
Rabia Clarke anakuwa mke wa nne kuolewa na Mandla Mandela, mjukuu wa kiongozi mwanzilishi wa Afrika Kusini huru Mzee Nelson Mandela.

0 comments:

Chapisha Maoni