Jopo la Wataalamu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Watu Wenye Asili ya Afrika (The Working Group of Experts on People of African Descent) limekutana na Wamarekani Waafrika au Wamarekani weusi kote Marekani na kutoa ripoti maalumu kuhusiana na mikutano hiyo.
Ripoti hiyo imebainisha wasi wasi mkubwa kuhusu kuendelea kukiukwa haki za Wamarekani weusi na kusema Wamarekani weusi wangali wanasakamwa na ile turathi ya utumwa, kukandamizwa, kutengwa na kubaguliwa hadi leo.
Jopo hilo limetoa wito wa kuundwa Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu ili kuchunguza kwa uwazi biashara ya watumwa waliotekwa Afrika na kupelekwa Marekani. Jopo hilo limesema biashara hiyo ya utumwa inapaswa kuangaziwa kama jinai dhidi ya binadmau. Kwa msingi huo, jopo hilo pia limependekeza kuwa, ili kuimarisha fikra zilizo dhidi ya ubaguzi wa rangi, kunapaswa kujengwa minara ya kumbukumbu kwa ajili ya kuwaenzi watu weusi kote Marekani. Aidha jopo hilo limependekeza kulipwa fidia Wamarekani Waafrika kutokana na jinai walizotendewa huko nyuma. Jopo hilo pia limebaini kuwa hadi sasa serikali ya Marekani haijawahi kuomba radhi kutokanana na jinai za zama za utumwa. Wajumbe wa jopo hilo la kimataifa wamesema wameshtushwa na dhulma na jinai wanazofanyiwa Wamarekani Weusi. Mwaka 2014, takribani asilimia 37 ya wafungwa wote wa magereza ya majimbo ya Marekani walikuwa ni weusi. Katika uchunguzi wake wa hivi karibuni, Banki Kuu ya Marekani imebaini kuwa Wamarekani wenye asili ya Afrika wana utajiri wa senti nane tu kwa kila mwanafamilia ikilinganishwa na wastani wa dola moja katika familia ya Wamarekani weupe. Aidha uchunguzi unaoneysha kuwa, zaidi ya nusu ya Wamarekani weusi huzaliwa katika dimbwi la umasikini. Kwa ujumla ni kuwa Wamarkeani weusi au wenye asilia ya Afrika wanaishi katika hali ya umasikini mkubwa wakilinganishwa na wazungu. Hata Wamarekani weusi walio katika tabaka la kati katika jamii, hali yao haiboreki kuelekea juu bali wengi wao wanaingia katika kundi la watu masikini.
Hali kadhalika mwishoni mwa mwaka 2014, Umoja wa Mataifa ulikosoa namna polisi wa Marekani wanavyoamiliana kinyama na Wamarekani weusi. Umoja wa Mataifa uliwataka viongozi wa Marekani kuchunguza ripoti za namna polisi nchini humo wanavyowashambulia watu wasio na silaha hasa Wamarekani weusi. Kamati dhidi ya utesaji ya Umoja wa Mataifa iliitaka Marekani kuchunguza kikamilifu ukatili wa polisi hasa mauaji ya kiholela ya Wamarekani weusi. Kamati hiyo ilibainisha wasiwasi wake mkubwa kuhusu kuendelea kuuawa kiholela Wamarekani weusi mikononi mwa polisi ya nchi hiyo.
Kwa msingi huo, Profesa Mireille Fanon-Mendes-France Mkuu wa Wataalamu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Watu Wenye Asili ya Afrika amesisitiza kuwa, jopo hilo lina wasi wasi mkubwa kuhusu hali ya haki za binadamu ya Wamarekani wenye asili ya Afrika. Ameongeza kuwa: "Historia ya ukoloni, turathi ya utumwa, ubaguzi wa rangi, ugaidi wa wenye misingi ya ubaguzi wa rangi na dhulma kwa msingi wa ubaguzi wa rangi Marekani ni changamoto kubwa. Hii ni kwa sababu hakuna uwajibikaji wowote wa kufidia na kuleta ukweli na maridhiano kuhusu Wamarekani wenye asili ya Afrika."
Aidha amesema kupewa kinga wanaotenda jinai za kiserikali ni jambo ambalo limeibua mgogoro wa haki za binadamu nchini Marekani na kwamba jambo hilo linapapswa kuchunguzwa na kutafutiwa ufumbuzi wa haraka iwezekanavyo.
0 comments:
Chapisha Maoni