Jumapili, Januari 24, 2016

RAIS MAGUFULI ATUNUKU KAMISHENI KWA MAAFISA WAPYA 205 WA JESHI PALE TMA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli jana tarehe 23 Januari, 2016 ametunuku kamisheni kwa Maafisa wapya 205 wa jeshi la wananchi kundi la 57/15 katika Chuo cha mafunzo ya kijeshi (TMA) Monduli Mkoani Arusha.
Maafisa hao wapya wametunukiwa cheo cha Luteni Usu, ambapo kati yao 16 ni maafisa wanawake, na 189 ni maafisa wanaume.
Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimpa zawadi mmoja wa wanafunzi aliyefanya vizuri O/Cdt. Mmang’anda katika Mafunzo .
Aidha, miongoni mwa maafisa wapya 205 waliotunukiwa kamisheni, maafisa 10 wametoka majeshi rafiki kutoka nchi za Uganda, Kenya na Burundi.
Akiwa katika uwanja wa paredi wa chuo hicho Rais Magufuli amepokea heshima zote za kijeshi ikiwemo kupigiwa wimbo wa Taifa na kukagua gwaride rasmi lililojumuisha maafisa hao wapya.
Baada ya kutunukiwa kamisheni, Maafisa wapya wa jeshi wamekula kiapo na wametoa heshima kwa gwaride lililopita mbele ya Rais kwa mwendo wa pole na mwendo wa haraka.
Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na maafisa wapya aliowatunuku Kamisheni pamoja na viongozi wa ngazi za juu wa Jeshi la Wananchi.
Viongozi wengine waliokuwepo katika tukio hilo ni pamoja na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange, Maafisa wa ngazi za juu jeshini na Maafisa wastaafu, viongozi wa mkoa na wilaya na wakufunzi kutoka nje ya nchi.
Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Magufuli kutoa kamisheni kwa Maafisa wapya wa Jeshi la wananchi tangu achaguliwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwezi Oktoba Mwaka jana.

0 comments:

Chapisha Maoni