Ndege isiyo na robani (drone) ya kipelelezi ya Jeshi la Wanamaji la Iran imeruka juu ya manowari yenye mitambo ya hali ya juu ya Marekani katika Ghuba ya Uajemi na kuchukua picha wakati wa luteka inayoendelea katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars, drone hiyo iliweza kuchukua picha za video wakati wa oparesheni ya kuipeleleza meli hiyo ya kisasa ya kivita ya Marekani.
Wakati huo huo, nyambizi ya wanamaji wa Iran ijulikanayo kama Ghadir nayo pia imefika karibu na manowari hiyo ya Marekani kwa lengo la kuipeleleza na pia kuchukua picha chini ya maji.
Imearifiwa kuwa nyambizi hiyo ya Iran imefanikiwa kuchukua picha safi pasina wanajeshi walioko kwenye meli hiyo ya kivita ya Marekani kutambua kuwa manowari hiyo ilikuwa inapelelezwa.
Siku ya Jumatano Jeshi la Majini la Iran lilianza mazoezi ya siku kadhaa katika eneo pana Ghuba ya Uajemi, Lango Bahari la Hormuz na Bahari ya Hindi, kusini mwa Iran.
Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Admeli Habibullah Sayyari amesema lengo la mazoezi hayo ya jeshi la majini la Iran yaliyopewa jina la ‘Velayat 94’ ni kudhihirisha uwezo wa kujilinda na chokochoko za maadui sambamba na kutuma ujumbe wa amani na urafiki kwa nchi za eneo hili kuwa vikosi hivyo vina uwezo wa kukabiliana na uvamizi wa maadui.
0 comments:
Chapisha Maoni