Alhamisi, Januari 21, 2016

MVUA ZA DAR ES SALAAM TAYARI ZIMEUA WANNE

MVUA zinazoendelea kunyesha nchini zimeendelea kuleta madhara baada ya watu wanne kupoteza maisha na wengine sita kujeruhiwa. Jijini Dar es Salaam mvua iliyonyesha kwa takribani saa tano mfululizo, ilisababisha athari kubwa hasa katika maeneo ya mabondeni pamoja na nyumba na barabara kujaa maji.
Hali ilikuwa mbaya jana majira ya asubuhi kutokana na mvua kubwa iliyoanza kunyesha tangu saa tisa usiku hadi saa tatu asubuhi. Mvua hiyo ilisababisha maeneo mengi, ikiwemo huduma muhimu kama barabara kujaa maji na kushindwa kupitika vizuri.
Katika eneo la Makumbusho Manispaa ya Kinondoni, njia ya kuingia kwenye kituo cha daladala ilijaa maji, kiasi cha magari kushindwa kupita, hali iliyosababisha msongamano mkubwa wa magari katika Barabara ya Morocco - Mwenge.
Aidha, katika maeneo ya mabondeni yaliyopo Barabara ya Kilwa kando ya mto Kizinga Manispaa ya Temeke, kutokana na mvua hizo moja ya madaraja ya barabara hiyo yalikatika na kusababisha maji na michanga kuingia kwenye nyumba zilizo kando na mto huo.

0 comments:

Chapisha Maoni