Ijumaa, Januari 15, 2016

MUME WA CELINE DION AFARIKI DUNIA, NDIYE ALIKUWA MANAGER WAKE

Rene Angelil, mume wa mwanamuziki mashuhuri duniani Celine Dion, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 73, nyumbani kwao Las Vegas nchini Marekani baada ya kuugua saratani ya koo iliyomsumbua tangu mwaka 2000.
Dion alichukua likizo kutoka kwenye muziki kwa vipindi viwili ili kumtunza Angelil baada kupatikana na saratani ya koo mwaka 2000.
Bw Angelil alizaliwa mjini Montreal mwaka 1942.
Baada ya kuwa meneja wa makundi kadha nchini Canada, aliombwa na wazazi wa Dion awe meneja wake mwanamuziki huyo alipokuwa na umri wa miaka 12 pekee.
Mwaka jana, Dion aliambia gazeti la USA Today kwamba alikuwa akijiandaa kwa kifo cha mumewe.
“Ikifika, itafika tu,” aliambia gazeti hilo Agosti 2015.
“Lakini kibarua change kikubwa kitakuwa kumwambia mume wangu kwamba tuko sawa. Nitawatunza na kuwalea watoto wetu. Utatutazama kutoka ulimwengu mwingine.”
Gazeti la Montreal Gazette linasema Bw Angelil aliweka rehani nyumba yake ili kupata pesa za kufadhili albamu ya kwanza ya mwanamuziki huyo.
Dion amerekodi albamu 25 studioni na ndiye mwanamuziki wa tano kwa kulipwa pesa nyingi zaidi, utajiri wake ukikadiriwa kuwa dola za kimarekani milioni 630 (sawa na euro milioni 437).
Mwaka 1999, wimbo wake My Heart Will Go On, uliotumiwa katika filamu ya Titanic, ulishinda tuzo mbili za Grammy.
Alianza tena kutumbuiza mashabiki wake mwaka jana baada ya kupumzika mwaka mmoja kumtunza Bw Angelil, ambaye aliacha kuwa meneja wake 2014.

0 comments:

Chapisha Maoni