Mji wa Randers ulioko katikati ya Denmark umepitisha uamuzi wa kulazimisha matumizi ya nyama ya nguruwe katika taasisi za umma zikiwemo shule za watoto wadogo.
Frank Nørgaard, mjumbe wa Baraza la Mji wa Randers amedai kuwa uamuzi huo umechukuliwa kwa madhumuni ya kuzuia kutoweka nyama ya nguruwe ambayo amesema ni 'sehemu kuu ya utamaduni wa vyakula vya Denmark'.
Denmark ni moja ya wazalishaji wakuu wa nyama ya nguruwe duniani, lakini kula nyama hiyo kumeharamishwa katika dini za mbinguni za Uislamu na Uyahudi.
Uamuzi wa kulazimisha ulaji wa nguruwe katika mji wa Renders umehusishwa na watu wanaoomba hifadhi ya ukimbizi nchini Demnark, ambao wengi wao ni Waislamu. Licha ya upinzani wa makundi ya kisiasa ya Denmark hususan ya mrengo wa kulia, idadi kubwa ya wakimbizi kutoka za nchi za Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika wamekimbilia nchini humo.
Frank Nørgaard, ambaye ni mmoja wa wapinzani wakuu wa upokeaji wakimbizi amedai kuwa uamuzi huo haulengi kuwakera na kuwaudhi Waislamu. Hata hivyo ameongezea kusema kuwa:"Ikiwa wewe ni Muislamu na una nia ya kuja Randers usitarajie kuwalazimisha watu wengine kutumia vyakula ulivyozoea wewe".
Hii si mara ya kwanza kwa Denmark kuchukua uamuzi unaokinzana na vyakula vilivyozoeleka kwa Waislamu. Itakumbukwa kuwa mnamo mwaka 2013, Waziri Mkuu wa wakati huo Helle Thorning-Schmidt, alivilaumu baadhi ya vituo vya kulelea watoto kwa kutumia nyama halali badala ya nyama ya nguruwe.
0 comments:
Chapisha Maoni