Makumi ya wahajiri wa Kisomali na Kiethiopia wamekufa maji baada ya boto yao kuharibika katika maji ya Somaliland kaskazini mwa Somalia.
Ahmad Abdi Falai mkuu wa eneo la Nasag huko Somaliland amethibitisha kufariki dunia wahajiri hao na kusema kuwa, boti mbili zilizokuwa zimewabeba wahajiri ziliondoka katika bandari ya Bossasso majuma mawili yaliyopita zikielekea kusikojulikana katika Peninsula ya Bara Arabu.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, viwiliwili 36 za wahajiri hao kutoka Ethiopia na Somalia vimekwishapatikana.
Afisa mmoja wa Shirika la Msalaba Mwekundu ameziambia duru za habari kwamba, bado kuna makumi ya watu wengine waliokuwa wakisafiri na boti hizo ambao bado hawajapatikana.
Inaelezwa kuwa, jumla ya wahajiri 106 walikuwa wakisafiri na boti hizo mbili kuelekea Peninsula ya Bara Arabu.
Wakati raia wa Somalia, na wale wa Somaliland na Puntland wamekuwa wakihajiri na kuelekea katika nchi nyingine kwa ajili ya kwenda kutafuta maisha, Wayemen ambao nchi yao inakabiliwa na mashambulio ya jeshi la Saudia na waitifaki wake wamekuwa wakiikimbia nchi hiyo na kuelekea huko Somalia.
Mara kwa mara kumekuwa kukiripotiwa matukio ya kupoteza maisha wakimbizi katika Pwani ya Somalia kutokana na wakimbizi hao kutumia boti na vyombo vya usafiri ambavyo havina viwango au boti hizo kupakia watu kupita kiasi.



0 comments:
Chapisha Maoni