Ijumaa, Januari 15, 2016

LOWASSA ATANGAZA KUWANIA URAIS 2020

Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania na aliyekuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA chini ya mwamvuli wa muungano wa vyama vya upinzani UKAWA, Edward Lowassa, amesema kuwa hajakata tamaa na ana nguvu za kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020.
Lowassa aliyasema hayo jana Alkhamis wakati alipokutana na viongozi tisa wa wafanyabishara wa Kariakoo wanaojiita 'Wapenda Mabadiliko' ambao walimtembelea ofisini kwake, na kuongeza kuwa, mwisho wa uchaguzi mmoja ni mwanzo wa uchaguzi mwingine.
Lowassa aliongeza kuwa bado miaka mitano kabla ya uchaguzi mwingine kufanyika na kwamba, muda huo si mrefu kwa maandalizi na kwamba maandalizi hayo tayari yameshaanza na amewataka wanachama wa chama cha CHADEMA kutokata tamaa.
Kwenye uchaguzi uliopita, Edward Ngoyai Lowassa alitajwa na wapinzani wake kwamba alikuwa na matatizo ya afya na kudai kuwa hawezi kuongoza nchi. Hata hivyo mtazamo wa Lowassa na wafuasi wake ni mwingine. Mwenyewe anasisitiza kuwa hajakata tamaa na ataendelea kugombea kwa sababu watu wanampenda.
Akizungumzia matokeo ya uchaguzi uliopita nchini Tanzania amesema, kama angepinga matokeo ya urais hadharani, basi kungetokea maafa makubwa kwa sababu anaamini alipigiwa kura zilizotosha kuwa rais wa Tanzania.

0 comments:

Chapisha Maoni