Ijumaa, Januari 15, 2016

BUHARI: TUMESHINDWA KUWAKOMBOA WANAFUNZI WA KIKE

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria ametangaza kukata tamaa juu ya kuwakomboa wanafunzi wa kike waliotekwa nyara na wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram nchini humo.
Hata hivyo Buhari amedai kuwa, jeshi la nchi hiyo limepata taarifa za kiintelejensia juu ya eneo wanakoshikiliwa wasichana hao.
Buhari aliyeyasema hayo jioni ya jana mbele ya mamia ya watu wa familia za wanafunzi hao, aliongeza kuwa, licha ya jeshi kuwa na ripoti hiyo ya eneo walipo wanafunzi hao wanaokadiriwa kuwa 200, lakini haliwezi kwenda kuwaokoa kutoka mikononi mwa wanachama wa Boko Haram
Zaidi ya watu 1000 wa familia za wanafunzi waliotekwa nyara na genge hilo la kitakfiri walikutana jana na rais huyo wa Nigeria huko Abuja, mji mkuu wa nchi hiyo, wakiitaka serikali yake kuhakikisha inawakomboa wasichana hao.
Hata hivyo rais huyo ambaye aliwapa matumaini mengi ya kulishinda kundi la Boko Haram raia wa Nigeria katika kampeni za uchaguzi uliomuingiza madarakani, aliwavunja moyo watu waliokutana naye baada ya kusema kuwa, licha ya askari kuwa na mafanikio makubwa dhidi ya magaidi hao katika majimbo ya Yobe, Adamawa na Borno, lakini haliwezi kuwaokoa mabinti hao.
Baadhi ya weledi wa mambo wanaamini kuwa, suala la Boko Haram linatumiwa na wanasiasa wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika kama daraja la kufikia malengo yao na kwamba serikali zote za nchi hiyo iwe ya rais wa zamani Goodluck Jonathan au ya hivi sasa, hazina nia ya kulimaliza genge hilo maarufu kwa kutenda jinai.

0 comments:

Chapisha Maoni