Fikiria gari lisilo na dereva sasa linatakiwa kufanya chaguo gumu--likigeuka upande wa kushoto, litagonga gari la SUV la Volvo; likigeuka upande wa kulia, litagonga gari lingine dogo la Mini Cooper. Kama ungetunga programu ya gari lisilo na dereva, utachagua nini ili kupunguza hasara?
Ukifikiri kwa mujibu wa fizikia tu, basi ni bora kugonga gari la SUV, kwa sababu hili ni gari kubwa zaidi, na linaweza lisiharibike sana kama Mini Cooper.
Lakini fizikia si suala pekee tunalohitaji kufikiria. Tukitunga programu kwa namna hii, maendeleo ya utengenezaji wa magari yasiyo na dereva yatafuata njia inayokwenda kinyume na sheria na maadili. Magari makubwa yatakuwa yanalengwa kugongwa mara kwa mara, lakini madereva wao hawajafanya makosa yoyote.
Hatuwezi kutegemea teknolojia ya kuzuia ajali zisitokee, kwa sababu baadhi ya ajali haziepukiki, kwa mfano, kuna tatizo la kiufundi au tatizo la sensa, hali ya hewa ni mbaya au bahati ni mbaya. Hivyo tunahitaji kufikiria mkakati wa kufanya uamuzi wa busara. Lakini inaonekana kwamba chaguo lolote haliwezi kuwaridhisha watu wote.
0 comments:
Chapisha Maoni