Waziri wa Fedha wa Kenya Henry Rotich amesema nchi yake inataka kujiunga na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC ili kuweza kupata mikopo nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Kiislamu (IDB).
Rotich amesema mipango inaendelea kutayarisha ombi la uanachama katika jumuiya hiyo ambayo ni ya pili kwa ukubwa baada ya Umoja wa Mataifa miongoni mwa jumuiya za kiserikali, ikiwa na nchi wanachama 57 zilizoenea kwenye mabara manne makuu ya dunia.
Waziri wa Fedha wa Kenya ameyasema hayo jana katika mkutano na waandishi wa habari baada ya kuongoza ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Kiislamu wa Fedha uliofanyika jijini Nairobi.
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ambayo inashughulikia zaidi maslahi ya mataifa ya Waislamu ina uhusiano wa kiushauri na kiushirikiano na Umoja wa Mataifa katika kutatua mizozo na migogoro inayohusisha nchi wanachama.
Ili nchi iweze kupata mikopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Kiislamu (IDB) yenye makao yake makuu mjini Jeddah, Saudi Arabia, inapaswa kuwa mwanachama wa OIC.
Akizungumzia nukta hiyo, Waziri wa Fedha wa Kenya amesema:” IDB imezipatia mikopo nchi nyingi za Afrika za eneo la Jangwa la Sahara, lakini Kenya bado haijawa mwanachama. Mara tu tutakapojiunga na OIC tutaweza kupata tahafifu kubwa za masuala ya fedha kama tunavyofanyiwa na Benki ya Dunia”
0 comments:
Chapisha Maoni