Jumapili, Januari 24, 2016

JINAI NA UHALIFU VIMEONGEZEKA UINGEREZA, WALES

Takwimu zilizotolewa zinaonesha kuongezeka kiwango cha jinai na uhalifu hususan vitendo vya mauaji katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita nchini Uingereza na Wales na kwamba, ongezeko hilo la uhalifu halijawahi kushuhudiwa katika historia ya nchi hizo.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya Uingereza imesema katika ripoti yake kwamba, vitendo vya mauaji yaliyofanyika katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita nchini Uingereza na Wales ni sawa na ongezeko la asilimia 14 ikilinganishwa na miaka ya nyuma. Taarifa zaidi zinasema kuwa, ongezeko la mauaji nchini Uingereza linashuhudiwa kwa mara ya kwanza katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.
Aidha kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya Uingereza, mji mkuu wa nchi hiyo London ndio unaoongoza kwa vitendo vya uhalifu ikilinganishwa na miji mingine ya nchi hiyo.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya Uingereza imetangaza kuwa, vitendo vya utumiaji mabavu dhidi ya watu katika jamii vimeongezeka kwa asilimia 27.
Gazeti la Daily Telegraph liliripoti katika toleo lake la jana Jumamosi kwamba, kuongezeka jinai na uhalifu nchini Uingereza chimbuko lake ni kupungua kwa polisi katika jamii ya nchi hiyo. Wakati huo huo, kuna ripoti zinazoonyesha kuwa maafisa wa polisi wanajihusisha na vitendo vya uhalifu.
Inaelezwa kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu ya hivi karibuni, kwa uchache maafisa 179 wa polisi nchini Uingereza wamepatikana na hatia ya kujihusisha na vitendo vya uhalifu kama vya ubakaji na dawa za kulevya.

0 comments:

Chapisha Maoni