Jumamosi, Januari 23, 2016

EWURA: BEI YA MAFUTA NCHINI KUSHUKA

EWURA imesema kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia kutaendelea kushusha bei hapa nchini LAKINI sio kwa wakati huohuo KWA SABABU hiyo bei watu wanayolalama ni ya mafuta ghafi na zaidi stock inayouzwa wakati husika siyo ile inayotajwa kwenye news break CNN, BBC kwamba imeshuka.www.ewura.go.tz, taarifa kamili hii hapa;

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU BEI ZA MAFUTA KATIKA SOKO LA DUNIA NA LA HAPA NCHINI​

1. UTANGULIZI

Mamlaka ya Huduma za Nishati na Maji (EWURA) inapenda kutoa taarifa halisi kuhusiana na mwenendo wa bei za mafuta katika soko la dunia na la hapa nchini. Kati ya majukumu ambayo EWURA imepewa ni kuweka bei KIKOMO za mafuta aina ya petroli katika soko la hapa nchini, utaratibu ulioanza rasmi Januari 6, mwaka 2009 baada ya kutokea hali ya kukosekana uhalisia wa bei za mafuta katika soko la ndani ikilinganishwa na mwenendo wa bei katika soko la dunia. Matokeo yake ni kuwa watumiaji mafuta walikuwa wakinunua mafuta kwa bei isiyo halisi (2,200/= kwa lita) katika miezi ya mwisho mwaka 2008, na pia uchumi wa nchi uliathirika na mwenendo huu wa bei. EWURA ilishusha bei hizo hadi kufikia 1,140/= baada ya kuanza kupanga bei mwezi Januari 2009.


Pamoja na kwamba bei za mafuta katika soko la dunia ndicho kigezo kikubwa cha upangaji wa bei katika soko la ndani, kuna gharama zinazoambatana na uagizaji mafuta hayo hapa nchini, kama vile gharama za usafirishaji, faida za waagizaji mafuta, kodi za Serikali, gharama za bandari na tozo za mamlaka mbalimbali nk. Kwa bei za Januari 2016, kwa mfano, mchango wa bei hizi za ndani unaochangiwa na bei za mafuta masafi katika soko la dunia ni: Petroli 46.60%, Dizeli 47.82% na Mafuta ya Taa 49.83%. Lazima ifahamike kuwa bei zinazooneshwa kwenye mitandao mbalimbali ni bei za Mafuta GHAFI (Crude Oil) ambayo yakisafishwa hutoa petroli, dizeli, mafuta ya taa na ndege, gesi ya kupikia (LPG), oil, lami n.k. EWURA inaweka bei hizi kwa kuangalia bei halisia ya mafuta yaliyosafishwa na si mafuta ghafi.

2. UHUSIANO WA BEI ZA MAFUTA GHAFI KATIKA SOKO LA DUNIA NA BEI ZA HAPA NCHINI

Mafuta ghafi (crude oil) yanaponunuliwa katika soko la Dunia inabidi yapelekwe kwenye viwanda vya kusafishia mafuta (refineries) ili kupata mafuta safi. Hatua hii huchukua takriban miezi miwili mafuta hayo kutufikia sisi kama walaji hapa Tanzania.

Bei za mafuta katika soko la ndani hukokotolewa kwa kutumia gharama halisi za uagizaji mafuta nchini ambazo hutokana na meli za mafuta yaliyopokelewa katika mwezi husika, ambayo huwa yamenunuliwa mwezi wa nyuma yake. Hivyo uhusiano wa bei za soko la dunia kwa mafuta masafi na za soko la ndani huwa ni kwa kupishana kwa miezi miwili kama inavyoainishwa na Jedwali Na. 1.0. Aidha, uhusiano wa bei za mafuta ghafi katika soko la dunia na bei za hapa nchini huwa ni kwa wastani wa miezi mitatu au zaidi.

Jedwali Na.1 Uhusiano wa bei za mafuta masafi katika soko la dunia na soko la ndani
Jedwali 1.PNG 

Bei za mafuta hapa nchini hupangwa na Mamlaka ya EWURA kwa kutumia kanuni (formula) maalum ambayo inatayarishwa kwa kuzingatia uhalisia wa vigezo husika. Aidha, utayarishaji wa kanuni hii huhusisha wadau wote na kisha kuchapishwa katika gazeti la Serikali baada ya kupitishwa na Bodi ya EWURA.

3. MWENENDO WA BEI ZA MAFUTA KWA SASA
Katika kipindi cha mwaka 2014 hadi Januari 2016 bei za mafuta katika soko la Dunia zimeendelea kushuka. Kushuka kwa bei za mafuta katika soko la dunia kutaendelea kushusha bei hapa nchini japo si wakati ule ule. Aidha ni muhimu kuzingatia kuwa bei za mafuta masafi katika soko la dunia huchangia takriban asilimia 46 mpaka 49 ya bei katika soko la ndani (kwa bei za Januari 2016), hivyo kushuka huko hakuwezi kuwa na uwiano wa asilimia mia na kushuka kwa bei

katika soko la ndani. EWURA itaendelea kutimiza wajibu wake kisheria katika sekta ndogo ya mafuta hapa nchini ikiwemo upangaji wa bei kikomo za mafuta, na pia kusimamia bei hizo katika maeneo yote nchini.

Ni vizuri ikakumbukwa pia kwamba hata hivi karibuni, bei za mafuta katika soko la Tanzania zimekuwa zikishuka kufuata mwenendo wa bei za mafuta katika soko la dunia kama ifuatavyo:
a) Bei ya petroli ilishuka toka kiwango cha juu zaidi, mwezi Septemba 2014, Shillingi 2,267 kufikia shillingi 1,898 kwa lita mwezi Januari 2016, hii ikiwa ni kupunguka kwa Shillingi 369 kwa lita.

b) Bei ya dizeli ilishuka toka kiwango cha juu zaidi, mwezi Aprili 2014, shillingi 2,149 kufikia shillingi 1,747 kwa lita mwezi Januari 2016, hii ikiwa ni kupunguka kwa shillingi 402 kwa lita.

c) Bei ya mafuta ya taa ilishuka toka kiwango cha juu Zaidi, mwezi Februari 2014 shillingi 2,069 kufikia shillingi 1,699 kwa lita mwezi Januari 2016. Hii ni sawa na punguzo la shillingi 370 kwa lita.

Punguzo hilo la bei limepatikana licha ya ongezeko la kodi ya Serikali la Shilingi 100 kwa lita ya mafuta na kushuka kwa thamani ya Shilingi ilishuka dhidi ya Dola ya Marekani ambapo katika mwaka 2015, thamani ya Shilingi dhidi ya Dola ilishuka kwa asilimia 30 toka Shilingi 1,729 kwa Dola ya mwezi Januari 2015 kufikia Shilingi 2,254 kwa dola mwezi Agosti 2015 na baada ya hapo thamani ya Shilingi imepanda kufikia Shilingi 2,158 mwezi Disemba 2015.

4. UZINGATIAJI WA KANUNI KATIKA KUKOKOTOA BEI ZA MAFUTA
Kanuni ya kukokotoa bei za mafuta ni ya wazi, siyo siri, na huandaliwa kwa mchakato ambao ni shirikishi na huhusisha wadau mbali mbali ikiwa ni pamoja na vyombo vya Serikali, wafanyabiashara wa mafuta na pia wawakilishi wa watumiaji wa mafuta. Kanuni inaelekeza kuwa kabla EWURA haijafanya mabadiliko yoyote ni lazima utaratibu huu uzingatiwe, isipokuwa kwa maamuzi ambayo yanapitishwa na Serikali, hususan kodi na tozo mbali mbali. Kunapotokea mabadiliko ya kodi au tozo za Serikali, EWURA hufanya mabadiliko husika mara moja, baada ya kupata waraka husika kutoka Serikalini.


5. HITIMISHO
Kushuka kwa bei za mafuta katika soko la dunia kutaendelea kushusha bei hapa nchini japo si wakati ule ule, kwamba yakishuka leo, kesho yanashuka hapa nchini.

Aidha kumekuwa na upotoshaji kwamba EWURA haishushi bei za mafuta kwa kuwa kushuka kwake kutaadhiri mapato yake. Ukweli ni kwamba tozo ya EWURA inatokana na lita za mafuta na si bei, kwa maana kwamba iwapo EWURA ingetaka mapato mengi, basi ingeongeza wingi wa lita za mafuta yanayoingia hapa nchini, na si kutegemea kupanda kwa bei. Hivyo basi kushuka au kupanda kwa bei hakuna uhusiano wowote na ongezeko la tozo kwa EWURA.

Imetolewa na Felix Ngamlagosi
Mkurugenzi Mkuu - EWURA

0 comments:

Chapisha Maoni