Sierra Leone leo (Alhamisi) imetangaza kugunduliwa kwa maambukizi mapya ya ugonjwa wa ebola baada ya shirika la afya duniani (WHO) kutangaza wiki iliyopita kumalizika kwa ugonjwa huo ambao umesababisha maafa katika mataifa ya Afrika magharibi tangu mwishoni mwa mwaka wa 2013.
Muathiriwa anasemekana kuwa jamaa wa karibu wa msichana mwenye umri wa miaka 22 ambaye alifariki kutokana na makali ya virusi vya ebola mapema mwezi huu katika kijiji cha Magburaka kilichoko wilaya ya Tonkolili. Hii ni maaambukizi mapya kuripotiwa tangu WHO kutangaza kumalizwa kwa ugonjwa wa ebola Afrika magharibi Januari 14.
Msemaji wa taasisi inayosimamia maswala ya ugonjwa wa ebola nchini Sierra Leone Yaya Tunis, alithibitisha kisa hicho huku akiongeza kuwa mgonjwa huyo anaendelea kupata matibabu katika hospitali moja ya kijeshi jijini Freetown. Tunis alisema kuwa muathiriwa alishika maiti ya jamaa wake kabla ya mwili hiyo kupimwa na kupatikana na virusi vya ebola.
0 comments:
Chapisha Maoni