Alhamisi, Januari 08, 2015

KENGE 149 WAKAMATWA UWANJA AIRPORT DAR .


Raia wa Kuwait, Hussain Ahmed Ally Mansour (34), amekamatwa na maofisa usalama na Jeshi la Polisi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa tuhuma za kutaka kusafirisha kenge hai 149 wenye thamani ya Sh. milioni 6.33 kwenda nchini Kuwait.
Tukio hilo la kusafirisha wanyama hai ni la pili kutokea nchini, la kwanza lilitokea mwaka 2010, baada ya twiga hai wanne waliosafirishwa kwenda nje katika mazingira yenye utata na hivyo kuzua mjadala ndani na nje ya nchi.
Kamanda wa Polisi Viwanja vya Ndege Tanzania, Hamis Seleman, alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa juzi saa 5:20 usiku akiwa ameficha kenge hao kwenye mifuko midogo 15 ndani ya begi jeusi kwa lengo la kuwasafirisha kwenda Kuwait kupitia Dubai kwa ndege ya Shirika la Emirates.
Alisema mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa na hati ya kusafiria yenye namba 003870237, alibainika akitaka kusafirisha kenge hao baada ya vyombo vya usalama katika uwanja huo kufanya upekuzi wa mizigo kabla ya abiria kuruhusiwa kuingia kwenye ndege.
Kamanda Seleman alisema baada ya kukamatwa, mtuhumiwa huyo alifikishwa katika Kituo cha Polisi cha Uwanja wa Ndege Dar es Salaam kwa ajili kuhojiwa ili hatua za kisheria zichukuliwe.

0 comments:

Chapisha Maoni