Ijumaa, Oktoba 31, 2014

TAREHE YA LEO KATIKA HISTORIA

Tarehe 31 Oktoba 1984 aliuawa Bi. Indira Gandhi, waziri mkuu wa wakati huo wa India. Mauaji hayo yalifanywa na walinzi wawili wa kiongozi huyo ambao walikuwa Masingasinga. Masingasinga hao walifanya mauaji hayo baada ya Gandhi kutoa amri ya kushambuliwa hekalu la dhahabu lililoko katika jimbo la Punjab, ambalo lilihesabiwa na masingasinga kuwa ni eneo takatifu. Masingasinga ambao wanaunda asilimia mbili ya watu wa India na wengi wao wanaishi katika jimbo la Punjab, walikusanya silaha zao kwenye hekalu hilo kwa shabaha ya kufanya uasi na kutaka kujitenga jimbo hilo.
Siku kama ya leo miaka 89 iliyopita, yaani tarehe 9 Aban 1304 Hijria Shamsia, Bunge la Ushauri la Taifa la Iran lilichukua uamuzi wa kumuuzulu Ahmad Shah, mfalme wa mwisho wa silsila ya Qajar na kukomesha kikamilifu utawala wa kizazi hicho nchini Iran kilichobaki madarakani kwa kipindi cha miaka 135. Baada ya kuondoshwa utawala wa silsila ya Qajar, Uingereza ilifanya njama za kuingilia kati na kuuweka madarakani utawala wa muda nchini ulioongozwa na Reza Khan. Reza Khan alijitangaza kuwa mfalme na kuanzisha silsila ya utawala wa Kipahlavi. Utawala huo wa Kipahlavi uliandaa mazingira ya kuporwa zaidi utajiri wa taifa na kukandamizwa wananchi wa Iran kulikofanywa na madola ya Uingereza na Marekani.
Na siku kama ya leo miaka 1030 iliyopita inayosadifiana na tarehe 6 Muharram mwaka 406 Hijria, alifariki dunia Sayyid Muhammad Hussein Musawi Baghdadi msomi mashuhuri, mwanafikra na mshairi wa Kiislamu. Aalim huyo pia alifahamika kwa jina la Sayyid Radhi. Alipata elimu za wakati huo katika kipindi cha ujana wake akuwa pamoja na ndugu yake, Sayyid Murtadha, ambaye pia alikuwa msomi mtajika. Sayyid Radhi aliinukia kuwa msomi mkubwa katika taaluma za Fiqhi, tafsiri ya Qur'ani Tukufu na elimu nyingine ya Kiislamu. Msomi huyo alikuwa wa kwanza kuasisi chuo kikuu kwa mtindo wa kisasa na ameandika zaidi ya vitabu 20 katika taaluma za fiqhi, tafsiri ya Qur'ani, historia na fasihii ya Kiarabu. Kitabu mashuhuri zaidi cha mwanazuoni huyo ni Nahjul Balagha ambacho kinakusanya semi, hotuba, amri, barua na mawaidha ya Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as).

0 comments:

Chapisha Maoni