Bunge maalumu la Katiba nchini Tanzania limepitisha rasimu ya katiba iliyopendekezwa.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya kura za ndio zilizopigwa na wajumbe kufikia kiwango kinachostahili.
Ili
katiba hiyo iliyopendekezwa ipite ilitakiwa kuungwa mkono na kura za
ndio theluthi mbili kutoka Tanzania bara na theluthi mbili za ndio
kutoka Zanzibar.
Jumla ya wajumbe wote wa bunge hilo la Katiba ni 629, huku 419 wakitoka Tanzania bara na 210 kutoka Zanzibar.
Zoezi
hilo la upigaji kura ambalo lilianza Septemba 29 mpaka Oktoba 2, siku
matokeo yalipotangazwa, lilisusiwa na wabunge wengi wa upinzani, kwa
madai kuwa baadhi ya vipengele vya awali vilivyopendekezwa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba iliyopewa kazi ya kukusanya maoni kutoka kwa
mwananchi, vilikuwa vimeondolewa.
Kabla ya kupitishwa kwa rasimu
hiyo, bunge hilo maalum la katiba lilikaa kama kamati kujadili
mapendekezo katika Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na tume hiyo ya
Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya uongozi wa Jaji Joseph Warioba.
Baada
ya kamati hizo za bunge hilo kutoa mapendekezo yao, kamati ya uandishi
ilikuwa na jukumu la kuandika upya Ibara za Sura za Rasimu ya Katiba
zilizojadiliwa na Bunge Maalum na hatimaye kutoa taarifa kwa Mwenyekiti
baada ya kukamilisha kazi hiyo.
Hivyo, Kamati ya Uandishi ilikuwa
na jukumu la kuhakikisha kuwa mapendekezo ya marekebisho, maboresho au
mabadiliko katika Rasimu ya Katiba yanakidhi matakwa na masharti ya
Kanuni za Bunge Maalum za Mwaka 2014.
Hatma ya katiba hiyo itahitimishwa kwa kura ya maoni inayotarajiwa kupigwa na wananchi.
0 comments:
Chapisha Maoni