Alhamisi, Septemba 25, 2014

TAZAMA WATOTO WANAVYOTUMIKISHWA VITANI

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umetangaza kuwa, makundi ya wanamgambo wanaobeba silaha yanawatumikisha maelfu ya watoto vitani nchini Sudan Kusini. 
Fatuma Ibrahim afisa mwandamizi wa UNICEF Sudan Kusini amesema kuwa, hivi sasa karibu watoto elfu kumi wako mstari wa mbele kwenye mapigano nchini humo. Fatuma Ibrahim ameongeza kuwa, makundi yanayobeba silaha yanawalazimisha kwa nguvu watoto kwenda vitani. 
Afisa huyo wa UNICEF amesema kuwa, makundi yanayobeba silaha nchini humo mwanzoni mwa mwaka huu yaliahidi kutowatumia watoto vitani, ahadi ambayo bado haijatekelezwa hadi sasa. Mwanzoni mwa mwaka huu, Umoja wa Mataifa pia ulizituhumu pande zote zinazopigana nchini Sudan Kusini kwa kuwatumia watoto wadogo vitani. 
Inafaa kuashiria hapa kuwa, kuanzia mwezi Disemba mwaka jana hadi sasa, Sudan Kusini inashuhudia mapigano makali kati ya wanajeshi watiifu kwa serikali ya Rais Salva Kiir dhidi ya wanamgambo waasi wanaoongozwa na Riek Machar makamu wa zamani wa rais wa nchi hiyo.

0 comments:

Chapisha Maoni