Wasomi mkoani Ruvuma,wamemtaja Abate
mstaafu Lambert Doerr OSB wa Abasia ya Peramiho kuwa ni Mwanahistoria wa
karne ya 21 kutokana na mchango wake mkubwa wa kuchangia shughuli
mbalimbali za maendeleo hapa Nchini ikiwemo katika nyanja ya Elimu.
Matamko hayo yalitolewa na Wasomi hao kwa
nyakati tofauti wakati walipokuwa wakitoa mada mbalimbali katika
kongamano lililoandaliwa kwa ajili ya kuzungumzia juu ya maisha na kazi
zilizofanywa na Abate huyo katika kipindi chake cha miaka 50 ya
Umisionari hapa Nchini lililofanyika kwenye ukumbi wa Nyerere chuo kikuu
cha Sauti tawi la Songea.
Akitoa mada katika kongamano hilo Padre
Dr.Xsaver Komba,alisema kuwa moja ya mchango wa uliotolewa na Abate
Lambert wakati akiwa Mwalimu bora na mwadilifu katika Seminari ndogo ya
Likonde na Seminari kuu ya Peramiho alifundisha kwabidii kwa kufuata
misingi ya ualimu iliyopelekea kutoa wasomi wengi ambao miongoni mwao
ni viongozi wakubwa wa Serikali na Dini.
Alisema kuwa michango mingine aliyoitoa ni
pamoja kuwaunganisha Waafrika kuwa kitu kimoja na wazungu kwenye nyumba
za kitawa, kuwasomesha baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mbinga Mharule
kwa kuwalipia ada ya shule,
kusogeza huduma ya maji safi na salama kwa
kilometa saba,kujenga zahanati,ujenzi wa barabara ya Lambert yenye urefu
wa kilometa tatu,kusaidia wazee wasiojiweza,watoto Yatima pamoja na
kuimarisha mahusiano kati ya dini ya kikristu na waislamu.
Alisema kuwa maadhimisho hayo ya Jubilei ya
miaka 50 ya Umisionari Nchini yatakwenda sambamba na na uanzishwaji wa
chuo cha ufundi cha Mtakatifu Lambert mjini hapa kitakachotoa fani ya
kompyuta,ushonaji na uselemala kama sehemu ya kumuenzi.
Naye mmoja wa watoa mada na mwanafunzi
aliyefundishwa na Abate huyo,Dr.Damas Mbogoro ambaye amewahi kushika
nyadhifa mbalimbali hapa Nchini alimwelezea Abate Lambert kuwa ni mtu
ambaye hakuwa mchoyo wa elimu na kudai kwamba alikuwa karibu na watu
katika kusikiliza shida na matatizo yao.
Kwa upande wake mgeni rasmi katika
kongamano hilo,Padre Dastan Mbano ambaye alimwakilisha Askofu mkuu wa
jimbo kuu katoliki la Songea Damian Dallu,alisema kuwa Abate Lambert ni
hazina kubwa sio kwa upande wa kanisa peke yake bali ni kwa jamii nzima.
Mbano alisema kuwa kazi nzuri na kumbukumbu
za Abate huyo zinapaswa kutangazwa,kuenziwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya
faida ya vizazi vijavyo huku mwakilishi wa Baraza la mila kasian
Shauritanga,alisema kuwa wamisionari
Wabenediktini wa Abasia ya Peramiho watakumbukwa kwa mchango wao wa
kusaidia kutunza kumbukumbu za mila na desturi za wangoni katika
makumbusho ya vita ya majimaji na kuupatia mkoa na taifa kwa ujumla sifa
pekee ya utunzaji.
0 comments:
Chapisha Maoni