Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amekosoa vikwazo ilivyowekewa Russia na
Magharibi kuhusiana na mgogoro wa Ukraine na kusema kuwa ni kinyume cha
sheria. Mugabe amesema vikwazo vinapasa kuidhinishwa kwanza na Umoja wa
Mataifa na kwamba vile ilivyowekewa Russia na nchi za Magharibi
havijapasishwa na umoja huo. Rais Mugabe na Sergei Lavrov Waziri wa
Mambo ya Nje wa Russia aliyeko ziarani nchini Zimbabwe jana walisaini
makubaliano ya uwekezaji ya dola bilioni tatu, ambapo Russia itachimba
madini ya platinamu huko Zimbabwe. Rais Mugabe amelaumu pia vikwazo
vipya vya Magharibi dhidi ya Russia ambavyo vimelenga katika sekta za
benki, nishati na ulinzi. Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa
Russia amesifu nafasi ya Afrika katika nidhamu mpya ya ulimwengu
sambamba na jitihada za Moscow za kuimarisha uhusiano na waitifaki wake
wa Afrika. Amesema kuwa Afrika ni moja ya nguzo za ukuaji wa mfumo wa
ulimwengu. Mgogoro wa Ukraine umesababisha kuvurugika uhusiano kati ya
Russia na nchi za Magharibi. Marekani na Umoja wa Ulaya zinaituhumu
Russia kuwa na ina mkono katika mgogoro huko mashariki mwa
Ukraine,tuhuma ambazo zimekanushwa na Moscow.
0 comments:
Chapisha Maoni