Jumatatu, Septemba 01, 2014

LEO KATIKA HISTORIA

Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita, kulifanyika kikao cha kwanza mjini Belgrade, Yugoslavia kwa kuhudhuriwa na viongozi wa nchi 25 wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM. Jumuiya hiyo ilikuwa na madhumuni ya kuunga mkono nchi za ulimwengu wa tatu dhidi ya kambi za Mashariki na Magharibi na sharti muhimu la kujiunga na jumuiya hiyo, ni kutokuwa na uanachama rasmi katika kambi hizo za Mashariki na Magharibi. Awali jumuiya hiyo iliundwa na pande mbili, upande wa kwanza ulikuwa upande usiokuwa kibaraka na wa kimapinduzi ulioongozwa na Tito, Ahmed Sukarno na Kwame Nkrumah, marais wa Yugoslavia, Indonesia na Ghana na Nehru Waziri Mkuu wa India ambaye alikuwa akipambana vikali na ukoloni. Ama upande wa pili, ulikuwa wa wahafidhina na wengi wao walikuwa wakifungamana na kambi za madola ya Mashariki na Magharibi. Kutofautiana nadharia kwa wanachama wa jumuiya hiyo ya NAM ni suala ambalo bado lipo hadi leo na kwa ajili hiyo, Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM haijaweza kuunda kambi yenye nguvu katika kukabiliana na madola ya kibeberu duniani.

Miaka 45 iliyopita mwafaka na leo, kulifanyika mapinduzi ya kijeshi nchini Libya yaliyomuingiza madarakani kanali Muammar Gaddafi. Kabla ya mapinduzi hayo, Libya ilikuwa ikiongozwa na utawala wa kifalme na mfalme Idris wa Kwanza. Wakati Idris alipoelekea nchini Uturuki kwa ajili ya matibabu, kundi moja la wanajeshi ambalo liliongozwa na Kanali Muammar Gaddafi lilifanya mapinduzi ya kijeshi na kumvua madaraka mfalme Idris wa Kwanza sambamba na kutangaza utawala wa kisoshalisti nchini Libya. Hata hivyo katika miaka ya kukaribia kupinduliwa na kuuliwa, Muammar Gaddafi alianza kufuata siasa za Wamagharibi na kuwakabidhi Wamagharibi viwanda vya mafuta vya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, hali inayodaiwa kuchangia hasira za wananchi na hivyo kutokea mapinduzi ya tarehe 21 mwezi Agosti 2011 dhidi ya utawala wa Gaddafi.

0 comments:

Chapisha Maoni