Jumamosi, Agosti 09, 2014

TID KUACHIA ALBUM YA 7, AMMANGA MR. NICE

Wakati idadi kubwa ya wasanii wa Bongo Fleva nchini wakikacha biashara ya kurekodi albamu na kutafuta njia mbadala ya kuuza muziki wao, mwanamuziki wa siku nyingi Khalid Mohamed maarufu (TID, Top In Dar), amesema anatarajia kutoa albamu yake ya saba.
Kwa mujibu wa TID albamu hiyo itatolewa hivi karibuni na itatambulika kwa jina la Mnyama na Wanyama the album.
Hatua hiyo ya Top In Dar ni kinyume na wasanii wenzake wa muziki ambao wengi wao wamegeukia mtindo unaokshika kasi wa kurekodi na wasanii wengine wa ndani, hata kimataifa (kolabo).
Njia hiyo hutumika kama mbadala huku pia ikilenga kuuza zaidi muziki wao na kutengeneza fedha za nje ya nchi kutokana na albamu kutouzika sokoni.
TID amejizolea umaarufu, akivuma kwa miaka kadhaa huku pia akitamba kwa albamu zake sita zenye nyimbo zilizobamba zikiwamo ‘Zeze’, ‘Mrembo’, ‘Girl Friend’ na ‘Siamini’.
Akizungumza katika mahojiano jijini Dar es Salaam, TID alisema:
Hivi karibuni nitaachia albamu yangu ya saba, ila kabla nitafanya bonge la ‘party’ Ukumbi wa Dar Live, Mbagala.
Anaitaja albamu yake ya Zeze ndiyo iliyokuwa ya kwanza ikifuatiwa  na Sauti ya Dhahabu, Burudani, Jembe, Sifai  na mwaka 2009 aliachia Prison Voice.
Anaeleza kuwa tangu hapo alipumzika hadi mwaka huu ndipo anatarajia kuiachia albamu yake ya saba, Mnyama na Wanyama the album.
Akieleza sababu za kukaa kimya kwa miaka minne bila kutoa albamu TID anasema:
Nilikuwa na mpango wa kuachia albamu mwaka huu, lakini kwa sababu siku hizi albamu ni tatizo kwa wasanii wengi na haziuzi, mimi nimefikiria ili niweze kuhimili vishindo vya tatizo hilo nimeona niboreshe kazi zitakazokuwa kwenye  albamu hii.
Anasema kuwa kufuatia changamoto hiyo ameamua kurekodi nyimbo nyingi zitakazoingia kwenye albamu hiyo ili kuondoa uwezekano wa maharamia kukopi albamu yake hiyo.
Zipo takriban nyimbo 25, lakini nimeona nichukue 18, zile nzuri zenye viwango. Nashangaa albamu ya Mr Nice ina nyimbo sita upande mwingine ni mdundo na upande wa pili ndiyo nyimbo zenyewe, mimi nimeamua kufanya kazi kwa bidii zote, albamu yote ina nyimbo zenye viwango
anasema.
TID anasema kwamba, hakuna kazi zitakazojirudia kwenye albamu hiyo ili kurudisha heshima ya albamu za wasanii wa muziki wa kizazi kipya.

0 comments:

Chapisha Maoni