Jumatano, Agosti 20, 2014

TAREHE YA LEO KATIKA HISTORIA


Siku kama ya leo miaka 16 iliyopita, yaani Agosti 20 mwaka 1998 Marekani ilizishambulia kwa makombora ya masafa marefu nchi za Sudan na Afghanistan. Serikali ya Washington ilidai kwamba, watu walioshiriki katika kulipua kwa mabomu balozi za Marekani mjini Dar es Salaam, Tanzania na Nairobi, Kenya wiki mbili kabla, walikuwa na uhusiano na nchi hizo. Aidha Washington ilidai kuwa ilikishambulia kwa mabomu kiwanda cha kuzalisha madawa cha ash-Shifaa nchini Sudan kwa madai kwamba kilikuwa kikitengeneza mada za kemikali. Hata hivyo weledi wa masuala ya kisiasa walisema kwamba, sababu ya Marekani kufanya mashambulio ya mabomu dhidi ya Sudan na Afghanistan ilikuwa ni kujaribu kufunika fedheha ya kimaadili iliyokuwa ikimkabili Rais wa nchi hiyo Bill Clinton. Kwa sababu hiyo mashambulizi hayo yaliamsha hasira za fikra za walio wengi na serikali nyingi duniani dhidi ya siasa za kutumia mabavu na kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za Marekani.

Miaka 36 iliyopita inayosadifiana na siku kama ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia wananchi wa mji wa Abadan kusini mwa Iran walifanya maandamano makubwa na kuonyesha hasira zao sambamba na kulaani hatua isiyo ya kibinadamu ya vibaraka wa utawala wa wakati huo wa Shah ya kulichoma moto jumba la sinema la Rex mjini humo. Katika tukio hilo la kinyama watu 277 wasio na hatia wakiwemo watoto na wanawake walipoteza maisha yao.

0 comments:

Chapisha Maoni