Alhamisi, Agosti 14, 2014

TAREHE YA LEO KATIKA HISTORIA

Siku kama ya leo miaka 8 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 14 Agosti 2006, yalimalizika mapigano kati ya harakati ya Hizbullah ya Lebanon na utawala wa Kizayuni wa Israel baada ya kutolewa azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lilikubaliwa na pande hizo mbili. Mapigano hayo yaliyoanzishwa na utawala wa Israel tarehe 12 Juni 2006, yalikuwa na lengo la kuidhoofisha na hata kuisambaratisha harakati ya Hizbullah. Kusimama kidete kwa wapiganaji wa Hizbullah dhidi ya majeshi ya Israel, kulimfanya Katibu Mkuu wake Sayyid Hassan Nasrullah apate uungaji mkono mkubwa kutoka ulimwengu wa Kiislamu. Baada ya kukabiliwa na mapambano makali ya wapiganaji shupavu wa Hizbullah askari wa Kizayuni ambao awali walikataa mpango wa kusitisha vita walilazimika kuukubali mpango huo na kurudi nyuma bila ya mafanikio yoyote.

Siku kama ya leo miaka 67 iliyopita, nchi ya Pakistan ilijitenga rasmi na India na kujitangazia uhuru wake. Dini tukufu ya Kiislamu iliingia Bara Hindi katika karne ya 8 na sehemu ya ardhi hiyo ambayo leo inajulikana kwa jina la Pakistan ilikuwa mikononi mwa Waislamu hadi wakati ilipokaliwa kwa mabavu na Waingereza mwishoni mwa karne ya 18. Chama cha Muslim League kikiongozwa na Muhammad Ali Jennah kiliundwa mwaka 1906 kwa lengo la kuunda serikali ya Kiislamu baada ya kuanza harakati za wananchi wa India dhidi ya mkoloni Mwingereza. Chama hicho kilifanikiwa kuwashawishi Waislamu wa India na hatimaye kiliunda nchi ya Pakistan.

0 comments:

Chapisha Maoni